RITA YAANZA KUSAJILI NA KUTOA VYETI VYA KUZALIWA MKOANI MWANZA. MULONGO ATETA JAMBO.
Naibu Waziri wa Katiba na sheria Mhe Ummy Mwalimu (Wa tano waliokaa) akiwa katika picha ya kumbukumbu na baadhi ya Wageni waliohudhuria uzinduzi wa Mkakati huo hivi karibuni Malaika Hotel Mkoani Mwanza.
Na:George GB Pazzo
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo
amewataka watumishi wa Afya Mkoani Mwanza kuhakikisha kuwa wanazingatia maadili
ya kazi yao, katika kuwasajili bure na kwa wakati watoto walio chini ya Umri wa
Miaka Mitano ili waweze kupatiwa Vyeti vya Kuzaliwa.
Hayo
yalibainishwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Zainab Telaki wakati akizungumza
kwa niaba yake katika Uzinduzi wa Kampeni ya siku saba ya Usajili na Utoaji wa
Vyeti vya Kuzaliwa bure kwa watoto waliochini ya Umri wa Miaka Mitano Mkoani
Mwanza uliofanyika Wilayani humo.
Alisema kuwa
watumishi wote katika Vituo vya Tiba watakaohusika katika Kampeni hiyo kuzingatia
utaratibu uliowekwa ambao ni pamoja na kuepuka vitendo vilivyo kinyume na
maadili ya utumishi wa Umma hususani vitendo vya Rushwa kwani zoezi hilo la kusajili
na kutoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio na umri chini ya Miaka Mitano
linaendeshwa bila malipo yoyote.
Nae Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini RITA Emmy Hudson
alibainisha kuwa Kampeni hiyo ya usajili
kwa watoto waliochini ya Umri wa Miaka Mitano itaendeshwa kwa muda wa siku saba
katika Wilaya zote Mkoani Mwanza.
Alisema
baada ya Kampeni hiyo kukamilika zoezi litaendelea katika Vituo vyote vya Afya
vipatavyo 282 Mkoani Mwanza ambapo takribani Watoto Laki tano na Elfu hamsini
na Mbili wanatarajiwa kusajiliwa na kupewa Vyeti Mkoani Mwanza.
Wakizungumza baada ya watoto wao kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, Rahel Charles Timba, Mzee Yohana pamoja na Magreth Kalist ambao wote ni Wazazi kutoka Wilayani Sengerema waliipongeza Serikali kwa kuendesha zoezi hilo bure na kuongeza kuwa wamefurahishwa zaidi kuona kwamba linaendeshwa katika Vituo vya Afya tofauti
na ilivyokuwa hapo awali ambapo Vyeti vya kuzaliwa vilikuwa vikitolewa katika
Ofisi za Wakuu wa Wilaya ambapo waliisihi Serikali kuangalia pia utaratibu wa zoezi kama hilo kufanyika kwa wananchi walio na Umri zaidi ya Miaka Mitano.
Kampeni ya
Usajili na Utoaji wa Vyeti kwa Watoto walio chini ya Umri wa Miaka Mitano
linasimamiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini RITA katika mfumo
wa teknolojia ya Internet ambapo usajili hufanyika na mtoto kupewa Cheti cha
Kuzaliwa papo hapo ambapo linaendeshwa katika Mikoa ya Tanzania bara.
No comments: