SITTA ATOA WITO KWA WANANCHI WA KATA YA WENDELE WILAYA YA KAHAMA MKOANI SHINYANGA.
(Picha haihusiani na Habari)
Na:Shaban Njia
Wananchi wa kata ya Wendele Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa kutokuingiza siasa katika miradi mbalimbali inayohusu maendeleo kwani kufanya hivyo nikuirudisha nyuma kata hiyo na taifa kwa ujumla kimaendeleo.
Wito huo ulitolewa wiki iliyopita na diwani wa kata hiyo Kilunga Sitta katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Tumaini kilichopo katani hapo na kusema kuwa ili maendeleo yawepo katika jamii, wananchi wanapaswa kuepuka upotoshaji unaoenezwa kwao na baadhi ya wanasiasa.
Sitta alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amefanikiwa kujenga Zahanati na nyumba ya mwalimu katika shule ya msingi Tumaini licha ya baadhi ya wananchi kutokushiriki katika shughuli hizo katika kutoa michango baada ya kupotoshwa na baadhi ya wanasiasa ili wasichangie.
Aidha aliwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kuonyesha ushirikiano kwa muda wote wa uongozi wake hususani wakati akisimamia miradi hiyo na kuwaomba kufanya hivyo kwa kiongozi ajae atakayeongoza kata hiyo ili miradi iliyopo iweze kukamilika.
Nao baadhi ya wananchi walimpongeza diwani huyo kwa kufanikisha ujenzi wa Zahanati katika kijiji hicho kwani ilikuwa ikiwalazimu kwenda umbali mrefu kufuata matibabu.
Mmoja wa wananchi hao Paul Lugata alesema kijiji hicho kilikuwa na tatizo la mawasiliano lakini juhudi za diwani huyo kuhakikisha mnara unajengwa zimefanikisha hilo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa mawasiliano na kurahisisha shughuli zao mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.
Hata hivyo wananchi hao walimchangia diwani huyo kiasi cha shilingi 25000 ili akachukue fomu ya kugombea Udiwani ili atetee nafasi yake katika kata hiyo.
No comments: