LIVE STREAM ADS

Header Ads

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU, KATIBU WA CCM KATA YA NYAMANORO MWANZA AWAPA SOMO VIJANA.

Judith Ferdinand
Vijana nchini wamehimizwa kutokuwa wepesi wa kuamini kile wanachoambiwa na wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo urais, ubunge na udiwani na badala yake watafakari kwa makini na kuwachagua viongozi wanaofaa bila kujali tofauti za vyama vyao.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Nyamanoro Bahati Ramadhani wakati akizungumza na Binagi Media Group katika ofisi za chama hicho Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.

Ramadhani alisema kuwa vijana wengi kwa sasa wameshindwa kutafakari na kuangalia kiongozi yupi anayeweza kuleta maendeleo, na  badala yake wamebaki kuwa mashabiki wa mtu mmoja na kumuaamini jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya taifa.

Pia alisema ili kupata kiongozi atakaye leta maendeleo nchini, vijana wanapaswa  kutafuta ilani za vyama vyote  ili kuzisikiliza, kuzisoma, kuzielewa na kuwauliza pale ambapo hawakuelewa, kisha  kuchambua ipi inayofaa na ipi isiyofaa.

“Kutokana na katiba ya nchi yetu haijaweka misingi ya uchumi zaidi ya ujamaa, vijana ambao ndio tegemeo kwa jamii mnapaswa kuangalia ilani ya chama gani itakayofaa katika suala la maendeleo ya watanzania na taifa kwa ujumla." Alisema Ramadhani.

Pia aliwataka vijana  na jamii kwa ujumla kutokubali kupandikizwa na kuaminishwa kuwa mfumo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni mbaya, na badala yake wawatake wanaotoa kauli hizo kutafsiri na kuthibitisha kwa vitendo na vielelezo kauli hiyo.

Hata hivyo aliiasa jamii kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaoona wanafaa kwa kuzingatia historia ya utendaji wao wa kuwatumikia wananchi.

No comments:

Powered by Blogger.