LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIONGOZI KATIKA SERIKALI YA AWAMU IJAYO WATAKIWA KUWAKUMBUKA WAZEE.

Na:Judith Ferdinand 
Wazee kutoka Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wamewaomba viongozi watakaobahatika kuingia madarakani katika serikali ya awamu ijayo kujenga desturi ya kutembelea wazee waishio vijijini ili kujua matatizo wanayokumbana nayo badala ya kukaa mjini pekee.

Wakizungumza jana wakati wa ziara ya kutembelea wazee vijijini iliyoratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wazee (MAPERECE) chini ya shirika la Help Age International walisema, wanataka kuwekewa mazingira bora yatakayowafanya waheshimike.

Walisema wamekuwaa waathirika kwa kufanyiwa vitendo viovu, ikiwemo kuuwawa kikatili kwa imani za kishirikina pamoja na kukosa matibabu ya uhakika kutokana na  ukosefu wa fedha kwa ajili ya  kumudu gharama za maisha.

Mmoja wa wazee hao aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya wenzake Tabu Basumaru alisema, wanahitaji usawa na haki ya kupata mahitaji ya msingi kutoka kwa jamii na mamlaka za serikali, pia viongozi watambue umuhimu wa wazee na hivyo kutoa matamko na kuchukua hatua za kulinda haki za wazee.

“tunakosa uwakilishi katika vyombo vya maamuzi na kilio chetu sisi tunamtaka Rais ajae aweze kuwa na sisi bega kwa bega ili heshima yetu irudi kama hapo awali”. alisema Basumaru.

Mageni Beregi ni mama aliyenusurika kifo kwa kukatwa mapanga baada ya kuvamiwa mwaka 2010 kwa tuhuma za kishirikina zinazo muhusisha   na vifo vya wazazi wake na kwamba yeye ndie mhusika wa mahuaji hayo.

Beregi alisema, tukio hilo lilitokea usiku wa manane wakati akiwa amelala nyumbani kwake Mwamala kijijini Sagani kata ya Nyigongo Wilayani humo ambapo alivamiwa na kukatwa mapanga kichwani.

Alisema kuwa  waliofanya kitendo hicho kuwa ni ndugu zake na alipofuata msaada wa polisi aliombwa kiasi cha pesa shillingi  10,000 kwa ajili ya  mafuta ya gari ili kuwafuatilia waliohusika na tukio hilo jambo ambalo alishindwa kulitekeleza kwa kukosa kiasi hicho.

Aidha alisema, kwa sasa maisha yake yamekuwa magumu kwa kuwa licha ya kupona amebaki kuwa tegemezi kwa kuwa hawezi kulima tena na kuvitaka vyombo vya usalama kuwafikisha  wahusika  katika vyombo vya sheria na kuwapatia adhabu kali ili kukomesha vitendo hivyo.

Salome Mfugo kutoka kijiji cha Lumeji alisema analishukuru shirika la Maperese kubuni miradi mbaliumbali kama utengenezaji wa sabuni za maji mafuta ya ngozi kwa lengo la kuwaondolea utegemezi kwenye familia. 

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Lumeji kata ya Sukuma Wilayani humo Enos Yohana alisema idadi ya vikongwe waliyo katwa mapanga toka mwaka 2009 kuwa  ni wanne huku wanawake wakiwa watatu na mwanaume mmoja.

Yohana alitazitaja sababu zinazopelekea kuwauwa kikatili kuwa ni imani za kishirikina, ugomvi wa mipaka, umasikini. maradhi pamoja na na ramli chonganishi kwa waganga wa kienyeji.

Alisema ili kukomesha vitendo hivyo waliweka mkakati wa ulinzi shirikishi kutoka kwa mabarozi wote ili kusambaza elimu kwa jamii nzima juu imani potofu waliyonayo kuwa vikongwe hao.

No comments:

Powered by Blogger.