LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAGOMBEA UBUNGE CCM WAPINGA MATOKEO WILAYANI SENGEREMA.


Na:Neema Emmanuel & Judith Ferdinand
Hali ya sintofahamu inaendelea kukikumba Chama cha Mapinduzi CCM, baada  ya Mkurugenzi wa uchaguzi jimbo la Sengerema kutangaza matokeo ya kura za maoni za ubunge ambapo aliekuwa Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Nishati na Madini William Ngereja aliibuka mshindi.

Katika Matokeo hayo, wagombea watano wameandika waraka wa kupinga ushindi wa Ngeleja katika jimbo hilo ambapo pia wanalalamikia utaratibu uliotumika kupiga kura za kumpata mgombea wa jimbo hilo.

Waraka huo umetumwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Abdurlahiman Kinana, pamoja na viongozi mbalimbali wa chama kwa ngazi ya Mkoa na Taifa akiwemo Makamu Mwenyekiti CCM (Bara) Phillip Mangula na Katibu CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu.

Joshua Shimiyu ni mmoja wa wagombea walioandika waraka wa kupinga matokeo ya kura za maoni ya ubunge katika jimbo hilo ambapo akizungumza kwa niaba ya wenzake  alisema kuwa zoezi la upigaji kura liligubigwa na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwemo kucheleweshwa kwa karatasi za kupigia kura katika baadhi ya kata.


“Kuna baadhi ya vituo mfano katika Kata ya Chifufu na Juma Kisiwani, karatasi za ubunge zilipelekwa mchana huku za udiwani zikipelekwa asubuhi hali iliyopelekea wananchama kupiga kura kwa upande wa diwani pekee na kuondoka". Alisema Shimiyu.

Shimiyu alisema kuwa kulikuwa na ukusanyaji wa madaftari ya wanachama kwa siri katika baadhi ya matawi ikiwemo Bitoto Kata ya Buyagu na Itonjambasa pamoja na  kuingiza majina ya wanachama wapya ili wampigie mgombea mwenzao aliyetangazwa kuwa ndiye mshindi.

Aliongeza kuwa alisikitishwa na kitendo kilichofanywa na Mwangalizi wa Uchaguzi huo (MNEC) Lameck Mahewa kwa kumtangaza aliekuwa mgombea mwingine ambae ni Lawrence Masha kuwa mshindi wa pili katika matokeo ya kwanza akitambua kuwa hakustahili kushika nafasi hiyo.

Alisema baada ya malalamiko yake kamati ilibaini ukweli wa matokeo na siku ya tarehe 3/8/2015 saa kumi jioni, ndipo matokeo yakatangazwa upya na yeye kuwa mshindi wa pili huku Masha akishika nafasi ya nne.

Wagombea wengine walioshiriki kuandika waraka huo ni  Anna Shija, Lawrence Masha, Musa Lugoye na Dr.Angelina Samike ambao ni miongoni mwa wagombea 13 waliojitokeza katika kinyanganyiro hicho akiwemo William Ngeleja ambaye alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 15,854 na kufuatiwa na Joshua Shimiyu aliyepata kura 3,951 na Philimon Tano akipata kura 3,603.

Malalamiko yaliyomo katika waraka huo yanaeleza kuwa kulikuwepo na vituo visivyo rasmi vya kupigia kura tofauti na maelekezo yaliyotolewa kuwa kila tawi la CCM litakuwa ni kituo cha kura.

“Tumeshuhudia  watu wasio na kadi za CCM wakiruhusiwa kupiga kura eti sababu walikuwa wamelipia kadi lakini walikuwa hawajapewa kadi zao na mfano ni katika kituo cha Mlaga Kata ya Buyuga, hii ni kukiuka kanuni za wagombea toleo la FEB,2010 Ib,13 kif (4)”. Alisema Shimiyu.

Malalamiko mengine yaliyoelekezwa katika kamati ya siasa ya Wilaya ni kamati hiyo kutozingatia jiografia na mazingira ya jimbo hilo, katika utaratibu wa mikutano ya kampeni, kwani ilifanyika kwenye kata hivyo kuwawia vigumu wanachama wengi kutoka katika matawi yao. 

Malalamiko hayo yalieleza kuwa hali hiyo ilipelekea wanachama kutopata fursa ya kufika na kuwasikiliza sambamba na kuwatambua wagombea hususani wapya katika kinyanganyiro hicho.

Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu alikiri kupokea malalamiko hayo ya kupinga matokeo ya kura za maoni ya ubunge kutoka kwa wagombea wa jimbo la Sengerema na kueleza kuwa takribani majimbo yote ya Mkoa wa Mwanza yametoa malalamiko ambayo alisema kuwa yanashughulikiwa na vikao vya ndani ya chama.

No comments:

Powered by Blogger.