LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEHEMU YA TATU: HATUA SITA MUHIMU MTU ANAZOTAKIWA KUPITIA ILI KUFANIKIWA.

Soma HAPA Sehemu ya Pili
MPANGO/KUPANGA
Mara ya mwisho tuliona kwamba katika hatua tano mtu anazotakiwa kupita ili kufanikiwa hatua ya kwanza ni KUAMUA na tuliandika japo kwa kifupi sana maana ya KUAMUA. Na tuliona hatua ya pili ambayo ilikuwa ni KUAMINI kile ulichoamua.Leo tunaangalia hatua nyingine ya tatu ambayo ni KUPANGA.
Nipo na kamusi yangu ninayoipenda ya Webster na nimeangalia maana ya Mpango inasema ni mkusanyiko wa vitendo ambavyo vinakuwa vimefikiriwa na mtu au watu kama njia ya kufanya au kufikia kitu fulani.
Raisi wa 16 wa Marekani Abrahamu Lincolin aliwahi kusema kwamba njia nzuri ya kutabiri wakati ujao utakuwaje ni kuutengeneza sasa. Njia pekee ambayo inamuwezesha mtu kutengeneza baadae ni kuwa na mpango sasa na si vinginevyo.
Watu wote waliofanikiwa katika maisha yao sasa ni ukweli usiopingika kwamba walikuwa na mipango kadha wa kadha ambayo iliwawezesha kufanya mambo yao na hivyo wakaweza kufanikiwa, ni dhahiri kwamba katika maisha huwezi kufanikiwa kama huna mipango. 
Na sio jambo la kishangaza kwamba watu ambao hawana mipango huwa wanatumiwa na watu wenye mipango, ukiwa mzembe katika kupangilia mambo yako basi jua fika kuna watu watakupangia na kukutumia katika mipango yao.
Kuwa na lengo alafu ukakosa mpango hakuna tofauti na mtu ambaye anatamani kitu alafu hajui namna ya kukipata kwa sababu kupitia mpango ndio mtu anaweza kujua ni namna gani anaweza kupata kitu fulani katika maisha yake.
Baada ya Kuamua kwamba utafanya kitu fulani katika maisha yako kisha ukakipangilia basi usije pia ukapoteza muda mwingi katika kupanga maana ukipoteza muda sana katika kupanga inaweza pia ikasababisha wewe kutoka nje ya kile ulichokiamua, baada ya kupanga mtu anatakiwa kuanza mara moja pasipo kupoteza muda mrefu. 
Hii ndio sababu mtu mmoja alisema kwamba mpango mzuri unaotendewa kazi leo ni bora zaidi ya mpango mzuri zaidi ambao utafanyiwa kazi kesho.
Usisahau kwamba kuna hatari ya watu wengine kukutangulia na wakaanza kufanya kile kitu ambacho ulikuwa unapoteza muda mrefu kwenye kukipanga, wewe na mimi ni mara ngapi tumeona mtu kafanya jambo fulani alafu akafanikiwa tukaanza kusema ooooooh jamani nilikuwa nataka kufanya hivyo hivyo lakini hili neno NILI kipindi hiki huwa halisaidii tena.
Lakini jee ni kipindi gani mtu anatakiwa kupanga? Mipango mizuri hupangwa wakati mtu hana hela kwa sababu akili ya mtu huwa inakuwa imetulia na inaweza ikafikiri zaidi, lakini pia watu wengi huwa hawana nidhamu pindi wanapokuwa na fedha hivyo kupanga wakati hawana fedha huwa inawasaidia sana, epuka tabia ya kusema nitapanga nikipata pesa nakuambia hutaweza kupanga maana badala ya kupanga utajikuta unatumia fedha zako, utashangaa ndio unaanza kuona kwamba makochi ni mabovu, sina flat screen sebleni, mara natakiwa kununua suti ya Italy, mara nlimwambia mama ntamnunulia kiwanja ukija kufungua macho fedha imeshaisha na hujafanya chochote ambacho kitakusaidia kuongeza fedha.
Nataka nikuambie kwamba sio kwamba haiwezekani kupanga kipindi una pesa inawezekana lakini jee wewe una nidhamu ya fedha maana ni watu wachache sana wanaweza kupanga kipindi wamepata fedha na hakika ni wale waliofanikiwa tuu ambao tayari wana hekima ya kutosha juu ya fedha tafiti zinaonesha ni mmoja katika watu kumi anayeweza kupanga kipindi amepata fedha je mimi ninaweza nikawa huyo mtu mmoja? Sasa ukishajiuliza hivi ndipo unaona umuhimu wa kupanga kabla ya kupata fedha.
Watu wote waliofanikiwa wana vyanzo vingi vya fedha Kiingereza vinajulikana kama MSI yaani Multiple sources of income, Je mimi na wewe tuna vyanzo vingapi vya fedha hili ni swali ambalo ni lazima ujiulize kila siku, je hii kazi ninayoifanya siku nikifukuzwa nna kitu kingine cha kuniwezesha nikaishi maisha ninayotaka, je hii biashara moja niliyonayo siku ikifa nitaweza kuishi maisha nayoyataka?
Mpango wako hakikisha utaonesha ni vitu gani utavihitaji ili kuutimiza, saa zingine unaweza ukawa na mpango fulani kwa mfano unataka kuwa mjasiriamali na hauna maarifa ya ujasiriamali hivyo itakubidi ukatafute maarifa hayo ili kuweza kutimiza mpango wako.
Baada ya kupanga mpango wako unatakiwa pia kujiuliza ni watu gani natakiwa kuwashirikisha katika mpango wangu huu na waandike kabisa kwenye mpango wako kisha mara moja anza mchakato wa kuwatafuta.
Pia weka makadirio ya fedha ambayo itahitajika katika mpango wako huo na bila kupoteza muda anza kufikiri njia mbalimbali ambazo unaweza ukazitumia ili kupata fedha ambayo itakuwezesha kuanza huo mpango wako.
Kuwa na mpango kutakusaidia sana katika maisha yako kwani mpango utakuonesha ni namna gani utaenda kutenda jambo fulani mpaka litimie. Kama hauna mpango inamaaanisha hujui utafikiaje kitu ambacho unataka kukifanya katika maisha yako.
Mpango pia utakusaidia kutokujihusisha na kila kitu maana saa zingine watu hawafanikiwi kwa sababu wanafanya kila kitu hii sio sahihi kuwa maalumu katika mambo fulani na sio kwenye kila kitu
Lakini pia kuwa na mpango mkubwa huwa kunavutia watu na utashangaa watu wanajitolea pengine hata kukusaidia maana wanakuwa wana shauku kubwa ya kuona namna ambayo utakavyotimiza mpango wako huo. 
Nataka ukimaliza kusoma hapa utoke ukachukue ule mpango wako uliouweka kwenye kabati na droo useme kwamba nimechoka kuairisha sasa ni wakati wa mimi kufanyia kazi mpango wangu siku moja naamini utanitafuta uniambie nilifanyia kazi mpango wangu na leo nimefanikiwa.
Itaendelea...

No comments:

Powered by Blogger.