LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIONGOZI WASISITIZA MATENDO BADALA YA MANENO KATIKA KULINDA MAZINGIRA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuonyesha uzalendo wa kweli kwa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira, hususan kupitia zoezi la upandaji wa miti katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa Januari 27, 2026, wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanafunzi, walimu na wananchi waliojitokeza kushiriki tukio hilo, Mheshimiwa Mpogolo amesema uzalendo wa dhati hauishii kwenye maneno bali unaonekana kupitia vitendo vinavyolinda rasilimali za taifa, huku akisisitiza kuwa mazingira ni msingi wa maisha na maendeleo endelevu.
“Rais Samia amekuwa kinara wa kampeni ya nchi ya kijani. Ni wajibu wetu sisi wananchi kuenzi maono haya kwa vitendo ili kulinda mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Mpogolo.

Katika kuimarisha utekelezaji wa wito huo, Mkuu wa Wilaya amewataka wakazi wa Ilala kuhakikisha kila kaya inapanda angalau miti mitatu, akisisitiza kuwa zoezi hilo linapaswa kuambatana na uangalizi na utunzaji wa miti hiyo ili iweze kukua na kutoa manufaa yaliyokusudiwa.

Aidha, amewaagiza wakuu wa shule na viongozi wa taasisi mbalimbali kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wa karibu wa miti inayopandwa katika maeneo yao badala ya kuishia kwenye kampeni za siku moja bila ufuatiliaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, amesema halmashauri imejipanga kutekeleza kikamilifu kaulimbiu inayosema “Uzalendo ni Kutunza Mazingira” kwa kupanda zaidi ya miti milioni moja katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Mabelya ameongeza kuwa pamoja na upandaji miti, halmashauri inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama mkakati wa kupunguza uharibifu wa misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Maadhimisho hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Ofisi ya Ikulu lililoelekeza jamii kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais Samia kwa kushiriki katika shughuli za kijamii zenye mchango wa moja kwa moja katika utunzaji wa mazingira, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kukabiliana na changamoto za tabianchi.

No comments:

Powered by Blogger.