LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAZEE WILAYANI MAGU WAIPONGEZA HOSPITALI YA WILAYA HIYO KWA KUANZISHA DIRISHA LA WAZEE.

Picha Kutoka Maktaba.
Judith Ferdinand
Wazee katika Wilayani Magu Mkoani Mwanza wameupongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuwatengea kitengo cha matibabu bila malipo baada ya awali kuteseka kwa kukosa huduma za matibabu.

Pongezi hizo zimekuja baada ya Shirika la kutetea haki za Zazee wilayani humo la MAPERECE linalodhaminiwa na shirika la Help Age International kuhamasisha hospitali hiyo kuwatengea wazee sehemu maalimu ya Matibabu.

Wakizungumaza na BMG kwa nyakati tofauti wazee hao walieleza kuwa hapo awali walikuwa hawapati huduma ya afya bure na kwamba walikuwa wakilazimika kutoa pesa ilihali kipato chao hakiwezi kumudu gharama za matibabu.

Walisema kuwa licha ya nchi nyingi kupitisha sera ya matibabu bila malipo kwa wazee, huduma hiyo imekuwa ni changamoto kubwa hususani barani Afrika ambapo wahusika hutaabika wakati wa kutafuta huduma za afya.

“Huduma hii ya matibabu tunayoipata katika hospitali ya Magu ni nzuri na tunahudumiwa vizuri lakini tunaomba serikali itulete wataalamu wa magonjwa ya wazee ili tuendelee kuhudumiwa vizuri’’. Alisema Yuritha John mmoja wa wazee katika Wilaya hiyo.  

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Magu John Kazimiri alisema kuwa hospitali yake inatoa huduma bure kwa wazee  wenye  umri wa miaka 60 na kuendelea japo wanakabiliwa changamoto ndogondogo ambazo zinahitaji utatuzi.

Naye Daktari wa kitengo cha wazee hospitalini hapo Mchamba Salimba alisema kuwa hospitali hiyo ilianzisha kitengo hicho baada ya kuona wazee wengi wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo  mifupa, moyo, kisukari pamoja na macho.

Aidha alisema kuwa hospitali hiyo inakabiriwa na changamoto ya kupokea wazee kutoka maeneo mbalimbali wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu hali inasababisha  kitengo hicho cha wazee kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa

"Tunaiomba serikali itenge bajeti ya kutosha kwa wazee ili waweze kupatiwa huduma ya matibabu bure kote nchini ikiwemo kuwapatia bima za miwani ili kuwasaidia wale wanaosumbuliwa na matatizo ya macho" Alisema Dr.Salimba.

No comments:

Powered by Blogger.