LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAKALA: MWANDISHI WA HABARI MAKINI NI CHUKIZO KWA UTAWALA WENYE MASHAKA.

Na:Denis Mpagaze
Siku moja baada ya mdahalo wa katiba ulioendeshwa na , Kituo kimoja cha Luninga nchini, Mh. Samuel Sitta alinukuliwa akisema,

“Nashangaa kuna chombo kimoja cha habari sijui kwa sababu ni binafsi,chenyewe ni midahalo tu,

sasa wameacha kutangaza mambo mengine,watu wanatukana tu,waziri Mkangara hebu tazama hili,nadhani na serikali inasikia huko”.
Maneno haya ni ishara ya kwamba Mh. Sitta amechukizwa. Nami nachelea kusema hii ni ishara ya utawala wenye mashaka.

Utawala wenye mashaka hutumia gharama nyingi kuhakikisha ubabaishaji wao haujulikani. Katika hili waandishi makini huwa ni chukizo kwao na huwindwa zaidi ya Tembo wa mbuga ya Ruaha, Iringa.

Angalizo! Sina maana kila mwenye kamera, kalamu na kipaza sauti ni mwandishi wa habari. Waandishi wa habari naowazungumzia hapa Tanzania wapo wachache sana usivyoweza kufikiria.

Waandishi wengi tulionao ni wahandisi wa habari au tuseme mamluki. Ndiyo hao ambao mpaka Benjamini Mkapa anaondoka madarakani aliwaita wavivu wa kufikiri, na wakati Rais Kikwete anawafananisha na kelele za mlango kwamba haziwezi kumzuia kulala. Kikwete bwana! Anamaneno!

Hapa nazungumzia waandishi wa habari makini. Waandishi wenye uwezo wa kuondoa serikali dhalimu madarakani hata iwe na nguvu kiasi gani kama alivyowahi kunena Tom Stoppard, mshairi kutoka London, “I still believe that if your aim is to change the world, journalism is a more immediate short-term weapon”. 

Bob Woodward na Carl Bernstein wa gazeti la The Washington Post mwaka 1972 waliangusha utawala dhalimu wa Richard Nixon, Rais wa Marekani enzi hizo, tukio ambalo leo hii linajulikana kama Water Gate Scandal. 

Waandishi hawa waliibua kashifa ya Rais Nixon ya kutaka kubaki madarakani kwa wizi wa nyaraka za siri kutoka kwa chama pinzani (National Democratic) katika jumba la Watergate mjini Washington. 

Nixon aliwachukia sana waandishi japo alishindwa awafanyeje. Pengine tukio hili la Watergate ndiyo lililowafumbua macho watawala wenye mashaka popote pale duniani wawachukie waandishi wa habari makini. 

Wakati nchi zilizoendelea wanafanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari kwa manufaa ya jamii, nchi zilizoshindwa kuendelea zinawaziba midomo waandishi kwa sheria kandamizi, vitisho na hata kuuawa. 

Ndiyo maana Thomas Jefferson, rais wa tatu wa Marekani alisema, “Ningeambiwa kuchagua kuwa na serikali bila magazeti au magazeti bila serikali nisingesita kuchagua jibu la mwisho”. 

Imani ya Jefferson hapa ni kwamba vyombo vya habari vinanguvu zaidi hata ya serikali. Ni kupitia vyombo vya habari jamii inaweza kushuhudia mgawanyo sawia wa rasilimali.

Amarya Seni amedhihirisha hili katika tafiti zake zote kwamba, hakuna nchi yoyote ile duniani yenye uhuru wa vyombo vya habari wananchi wake wakafa kwa njaa. 

Tanzania tunanjaa kwa sababu waandishi hawako huru. Leo mwandishi makini akianza kufuatilia uozo unaofanywa na watawala dhalimu basi kesho asubuhi usishangae kukuta amenyofolewa kucha, ameng’olewa meno kwa ‘magalo’, ametobolewa jicho kwa spoko ya baiskeli na kuchinjwa kama kitoweo cha mwaka mpya. 

Ni ishara ya utawala wenye mashaka. Sun Tzu mnamo miaka ya 400 aliita kitu hii "Kill one, terrify a thousand". Ni ‘style’ karibu katika nchi zote zilizoshindwa kuendelea kama ya kwetu. Ngoja nikupe mifano miwili mitatu hivi. Tarehe 22 Novemba 2000 mwandishi wa habari makini, Carlos Cardo, alipigwa risasi huko mjini Maputo Msumbiji akiwa katika harakati za kuchapisha kwenye gazeti lake Metical ubadhirifu wa dola za Kimarekani milioni 14 kwa ajili ya maendelea kutoka benki kuu, “Banco Comercial de Moçambique”.

Miongoni mwa wabadhirifu wa pesa hizo ni Nyimpine Chissano yaani mtoto wa aliyewahi kuwa mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim, Joaquim Chissano na mke wa Chissano. Habari kutoka Mozambique News Agency AIM zinasema Nyimpine Chissano aliachiwa huru kwa sababu ya nguvu ya baba yake. 

Mwandishi mwanamama machachari, Anna Politikovskaya alimnyima usingizi rais wa Russia Vladimir Putin kwa kitendo chake cha kuivamia Chechnya mwaka 1999. Cha kusikitisha Anna aliuawa siku ya “Birthday” ya Putin mwaka 2006. 

Na mfano wa mwisho ni wa mwandishi kutoka Congo DRC, Frank Ngyke Kangundu, na mke wake Helene Paka waliuawa mjini Kinshasa mwezi Novemba 2005 baada ya kuchapisha habari kuhusu ubadhirifu uliofanywa na Joseph Kabila kwa kuficha dola za kimarekani milioni 30 nchini Tanzania. 

Ninachotaka ni kuwakumbusha waandishi wenzangu kwamba kazi nzuri wanazozifanya ni chukizo kwa utawala wenye mashaka, kwa hiyo kinachotakiwa ni juhudi binafsi za kujilinda.

Nikirejea maneno ya rafiki yangu na mwanaharakati, Donald Kasongi, kwamba “hakuna habari inayozidi uhai wako”. Hofu kwa watawala wenye mashaka haikuanza leo.

No comments:

Powered by Blogger.