MGOMEBA NCCR MAGEUZI AAHIDI KUTOA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI BURE.
Na:Shaban Njia
Mgombea Udiwani kwa tiketi ya Chama cha NCCR Mageuzi katika kata ya Mhongolo Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga Godwin Tumsime amesema kuwa ikiwa atapata ridhaa ya kuwa diwani wa Kata hiyo atahakikisha anasimamia vyema upatikanaji wa msaada wa kisheria hususani juu ya migogoro ya ardhi katika kata hiyo.
Tumsime alitoa kauli hiyo juzi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mtaa Igadiga na kuongeza kuwa kwa kutumia taaluma yake ya Sheria aliyosomea atakuwa Msaada mkubwa kwao pindi atakachopata ridhaa ya kuwaongoza.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka ya nyuma Wananchi wa kata hiyo walikuwa wakipata shida katika masuala mazima ya kisheria na kuongeza yeye ni mtaalamu wa Sheria na ataweza kuwasaidia katika migogoro mingi ya ardhi iliyopo katika kata hiyo.
Aidha Mgombea alisema kuwa atahakikisha kuwa Viwanja vinapimwa katika kata yake ili kupata maeneo muhimu ya huduma za kijamii kama vile maeneo ya Shule, Zahanati pamoja na maeneo muhimu ya mziko na kuondoa adha ya kwenda kuzika katika kata ya jirani ya Malunga.
“Lazima tupate maeneo kwa ajili ya Shughuli za kijamii kama maeneo ya maziko, ipo siku mtakwenda kuzika katika kata jirani ya Malunga na kuzuiliwa na Wananchi kwa kwa kuwa sio eneo la maziko kwa ajili ya Wananchi wa Kata ya Mhongolo”. Alisema Tumsime.
Hata hivyo Tumsime alisema kuwa zile fedha za asilimia tano kwa akina mama pamoja na nyingine kwa akinababa zinazotolewa na Halmashauri ya Mji kwa Vikundi hivyo zinawafikia Walengwa ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Halmashauri kujenga miundombinu ya maji katika kata hiyo.
Tumsime alisema kuwa ameamua kuogombea Udiwani katika kata hiyo kutokana na kuona kuna Changamoto zaidi ya tano katika maeneo hayo na kuzitaja kuwa ni pamoja na upimaji wa Viwanja, Asilimia tano ya fedha za Halmashauri, Ujenzi wa Mabweni katika shule za sekondari,kuiweka kata hiyo katika ramani pamoja na ujenzi wa Zahanati.
No comments: