LIVE STREAM ADS

Header Ads

UTOAJI WA ELIMU NA USHAURI KWA WAGONJWA WA MAJUMBANI WASAIDIA KUPUNGUZA MAUAJI KWA WAZEE.

Picha kutoka Maktaba
Judith Ferdinand, Mwanza
Imeelezwa kuwa utoaji wa elimu na ushauri kwa mgonjwa nyumbani kuhusu kupima afya, imesaidia kupunguza imani potofu za kishirikina katika jamii ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji ya wazee wenye umri mkubwa.

Hayo yalisemwa jana na Hermenegild Mganga ambae ni Mwenyekiti wa kitengo cha Wahudumu kwa Mgonjwa Nyumbani (Home Basic Care-HBC)kilichopo chini ya Shirika la Maperece la Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza ambalo linalojishughulisha na utetezi wa haki za wazee kwa kushirikiana na Shirika la Help Age International.

Alisema kutoa elimu pamoja na ushauri kwa wagonjwa walioko nyumbani sambamba na wanaoishi na wagonjwa hao kuwapeleka  hospitali kupima afya, kumesaidia kupunguza imani potofu za kishirikina ambazo zimekuwa chanzo cha mauaji ya wazee wenye umri mkubwa na wengine kukatwa mapanga.

"Kazi yetu ni kuwashauri wagonjwa walioko nyumbani waende hospitali na waache imani potofu za kishirikina ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji ya wazee wenye umri mkubwa na wengine kukatwa mapanga, hata hivyo tunawashauri wanaoishi nao kwa sababu wao ndio wahusika wakuu, hii imesaidia kuwepo kwa upungufu wa imani hizo katika jamii". Alisema Mganga.

Aidha alisema, katika kitengo hicho kuna wahudumu 100 ambao kila mmoja anawastani wa kuhudumia wagonjwa watano au zaidi ambao wamekua wakiugulia nyumbani kwa kuwatembelea na kuwapa ushauri.

Pia katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu alisema, anaamini katika Wilaya hiyo wazee wengi watashiriki katika zoezi la kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaokuwa kwa ajili ya manufaa yao kutokana na kuwekwa kwa vituo vingi vya kupigia kura na kupewa kipaumbele kuwa moja wapo katika makundi maalumu.

Akiongea kwa niaba ya wagonjwa hao, Raphael Misuka, alisema kabla hajaanza kuhudumiwa na HBC hali yake ilikuwa mbaya zaidi kwa kukosa matibabu ya dawa kutokana na ugonjwa wa kisukari anaoumwa, lakini tokea ameanza kuhudumiwa hali yake imebadilika kwani amekuwa akipata tiba nzuri kwa kupata dawa nyingi hata akiwa hana pesa.

Kwa upande wa mmoja wa wahudumu wa HBC, Lucas Buganda alisema kuwa suala la umasikini lilikuwa likichangia wengi wao wasiweze kufika hospitali hivyo elimu na ushauri wanaoutoa umeweza kuboresha na kufanikisha muitikio wa huduma kuongezeka.

Nae Mratibu wa Mradi wa Afya bora kwa wazee wa Shirika la Maperece Grace Julius, alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuhakikisha wazee wanapata huduma rafiki za afya hivyo kupitia kitengo hicho huduma  hizo zimeboreshwa baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu kukubali kutenga kitengo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wazee.

No comments:

Powered by Blogger.