MWIGULU NCHEMBA AWAONYA WAPINZANI WANAOTUMIA FALSAFA ZA MWL.NYERERE KUOMBA KURA.
Picha kutoka Maktaba
Na:Shaban Njia
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi CCM Mwigulu Nchemba amewaonya wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wanaotumia kauli ya baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere kuwa wasipopata mabadiliko ndani ya CCM watayapata nje ya CCM kwa kuwa wanaipotosha jamii.
Nchemba alitoa kauli hiyo juzi wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi Mkoani Shinyanga katika mikutano mbalimbali ya hadhara aliyoifanya katika majimbo ya Kahama Mjini, Ushetu pamoja na jimbo la Msalala iliyokuwa imelenga kuwanadi wagombea wa chama hicho.
“Ni Kweli Mwl.Nyerere alisema kuwa msipopata mabadiliko ndani ya CCM mtayapata nje ya CCM na CCM inaweza kuwaletea mabadiliko hayo ndio maana tunawaletea wagombea makini John Pombe Magufuli, ambae anaweza kupambana na rushwa wakati akiwa Ikulu”. Alisema Nchemba.
Aliongeza kuwa Mabadiliko ambayo watanzania wamekuwa wakiyataka sio ya vyama vya siasa bali ni ya utendaji bora wa kazi hali ambayo itaweza kubadili maisha yao na hivyo kuinua uchumi wa nchi kwa kufanya kazi kwa bidii.
Nae Mgombea Ubunge Jimbo la Kahama Mjini (CCM) Jumanne Kishimba aliwataka Wananchi wa Jimbo hilo kumuamini kuwa yeye ni kiongozi atakayeweza kuleta maendeleo katika jimbo la Kahama Mjini pindi atakapopata ridhaa ya kuwa mbunge.
No comments: