LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEHEMU YA TANO: HATUA SITA MUHIMU MTU ANAZOTAKIWA KUPITIA ILI KUFANIKIWA.

Soma HAPA Sehemu ya Nne
5.HATUA YA TANO NI KUENDELEA.
Baada ya kuanza hatua inayofuata ya muhimu ni KUENDELEA, Ni dhahiri kwamba kuanza hakuna maana kama mtu hutaendelea kutenda hicho ulichoanzisha. 
Tunaanza kutenda kitu ili tuendelee mpaka mwisho. Siyo kuanza na kuacha, ni bora usianze kabisa kama unajua hautaendelea maana utapoteza muda na fedha zako bure. Namna nyingine ya kusema maneno haya ni kwamba hautakiwi kuwa na msamiati wa ninajaribu bali unatakiwa kuwa na Yes au No, nitafanya au sifanyi basi.
Kuendelea nakuzungumzia hapa ni kuendelea kufanyia kazi kile ambacho umekianzisha kwa namna ya kiutendaji na jinsi ambavyo unatoa huduma zako kwa watu. Ngoja nikuambie, kukata tamaa kunaanzia wapi kwenye maisha. Kukata tamaa kunaanzia pale ambapo kunakuwa hakuna maendeleo katika kile ambacho mtu anakuwa anakifanya, maisha ninayoongelea hapa ni maisha kulingana na kile unachokifanya.
Mtu anapoendelea kufanya kitu alichoanzisha inamaanisha kuwa anazidi kupata motisha wa kile ambacho anakitenda, motisha huwa una tabia ya kuisha kama huendelei kufanya kitu ambacho umekianzisha.
Lakini ni nini kinamfanya mtu anaendelea kufanya kile alichokianzisha? sababu kubwa ni kwamba anakuwa anaamini kwamba kile ambacho anafanya ni sahihi na kitaleta mabadiliko kwenye jamii yake na kwake mwenyewe, kwa hivyo basi watu wote ambao huwa wanaanzisha vitu alafu wakashindwa kuendelea huwa hawaamini kwamba kile wanachokuwa wameanzisha ni sahihi na kama kitaleta mabadiliko.
Kwa kawaida Watu ambao wana mtazamo chanya na wanaopenda maendeleo yako hupenda kukuona ukiendelea kufanya kile ambacho umekianzisha siku zote, huduma na bidhaa ambazo umeanzisha hupenda waje kununua kwako, wanataka kuona ukiendelea kufanya ulichoanzisha siku hadi siku. 
Watu wengine pasipo kujua huwa wanaanzisha kitu fulani kisha wanatoa huduma vizuri inatokea tatizo kidogo tu labda tuseme mtaji kisha wanajikuta wanakatisha huduma sehemu ile jambo ambalo si sahihi, unachotakiwa kama kweli wewe umenuia kufanya hicho unachokifanya ni kutafuta namna ya kupata hicho kilichopungua ila sio kuacha kuendelea kutoa huduma.
Wateja wanapenda wakianzishiwa kitu kizuri waone kinaendelea ili hata kesho wakija tena wapate huduma nzuri kama waliopata jana yake na siku zingine, hii huwa inawafanya watengeneze imani kwako na kwa huduma ambazo unatoa tofauti na mtu ambae anaanzisha na kushindwa kuendelea kutoa huduma.
Kwa mtu kuendelea kufanya jambo ambalo ameanzisha kunamsogeza na hatua ya Sita ya muhimu ambayo ni MAFANIKIO,watu wengi hawajui kwamba mafanikio ni mjumuiko wa vitu vidogo vidogo ambavyo vinakuwa vinafanywa kila siku kwa ufanisi na umakini wa hali ya juu. Huwa wakimuona mtu aliefanikiwa akiwa juu huwa hawataki kuangalia ni mambo gani aliyafanya nyuma kabla hajafika hapo alipofika.
Ili kuweza kuendelea, unahitaji nidhamu na kujitoa kwa hali ya juu, nidhamu ni uwezo wa kuweza kutawala akili na mwili, kama kuna vitu uliwaanzishia watu kipindi umeanza unatakiwa kuendelea kuwafanyia kila siku katika kiwango kile kile na wasihisi kupungukiwa huduma wala bidhaa kwako.
Wewe uliefungua hoteli ukaanza kwa kutoa huduma nzuri na safi, wateja wakazipenda wakaanza kuja, unatakiwa kuendelea kuhakikisha huduma inaendelea kuwa katika hadhi ya juu, vivyo hivyo mtu asije akahisi kupungukiwa au kumetokea badiliko la kiutendaji.
Ikiwa ulianza kwa kufungua duka lako kila siku saa kumi na mbili na nusu na watu wanajua muda huo unakuwa umefungua duka, endelea kufanya vivyo hivyo sio unafungua siku nyingine saa tano mara saa saba hueleweki endelea kama ulivyoanza kama ulianza vizuri ila kama ulianza vibaya basi huna budi kubadili namna unavyotenda mambo yako.
Ulianza kwa kuongea vizuri na wateja wako usibadili kauli mara leo unaongea vibaya mara kesho vizuri itakupotezea wateja wengi sana maana watakuwa hawakuelewi wewe ni mtu wa aina gani, wateja wanapenda kusikilizwa, kuthaminiwa na kupatiwa huduma nzuri.
Endelea kufanya ulichoanzisha maana ndio njia pekee ya wewe kufikia lengo lako katika maisha, watu waliofanikiwa katika maisha walianzisha kitu fulani wakaendelea kukisimamia na kukifanya mpaka wakafika katika hatua ya mafanikio, jua kwamba mafanikio huja kwa kuendelea kufanya vitu ambavyo umeanzisha. Mafanikio ni matokeo ya kuendelea kufanya kila siku kwa ari na nguvu mpya.
ITAENDELEA...
USISITE KUSHEA UJUMBE HUU NA RAFIKI ZAKO UNAOWAPENDA. Imeandaliwa na LIFE SECRETS COMAPNY, MWANZA.

No comments:

Powered by Blogger.