LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWILI WA MAWAZO SASA KUAGWA JIJINI MWANZA.

Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza leo imefuta agizo la Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, ambalo lilikuwa linazuia kufanyika kwa shughuli za ibada ya kuuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Geita, Marehemu Alphonce Mawazo alieuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana Novemba 14 mwaka huu Mkoani humo.

Zuio la Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza lililotolewa na Kamanda wa jeshi hilo Charles Mkumbo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa madai ya kuwepo na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, hatua iliyosababisha Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mlezi wa Marehemu Mawazo kwa kuungwa mkono na Chadema kufungua kesi ya msingi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ili kuiomba mahakama hiyo kuondoa zuio hilo.

Baada ya Mawakili wa pande zote mbili zilizokuwa zinahusika katika kesi hiyo ambayo ilifunguliwa juzi, Jaji wa Mahakama hiyo Lameck Mlacha akaamua kutengua zuio la polisi alilosema kuwa halikuzingatia haki.

Kufuatia maamuzi hayo, Mahakama ikashauri kuwa ni vyema ndugu wa marehemu Mawazo wakashirikiana na Chadema pamoja na jeshi la polisi ili kuratibu shughuli za ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo kwa ajili ya kuhifadhiwa, ikizingatiwa kwamba ni takribani siku 12 mwili huo umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa Bugando.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe amesema kuwa maamuzi hayo yataheshimiwa na kwamba taratibu za kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo zinafanyika ili ikiwezekana mwili huo uweze kuagwa kesho ijumaa Jijini Mwanza.

Inje ya viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, ilikuwa ni nderemo na vifijo baada ya Mahakama kutoa hukumu ya kesi hiyo ambayo imevuta hisia za wakazi wengi wa Jijini hapa huku hali ya ulinzi na usalama wa polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa na silaha za moto pamoja na mabomu ya machozi ikiwa imeimarishwa kila kona Jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.