TAASISI YA BILAL MUSLIM YAZISAIDIA FAMILIA TANO MKOANI MWANZA KUANZISHA MIRADI YA UFUGAJI.
Na Judith Ferdnand ,Mwanza
TAASISI ya The Bilal Muslim Mission of Tanzania, imetoa msaada wa mbuzi 50 wenye thamani ya sh.2.5 milioni kwa familia tano maskini zenye vipato duni katika Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza ili zianzishe miradi ya ufugaji itakayozisaidia kuinua uchumi wao na kuboresha hali zao za maisha.
Msaada huo ulikabidhiwa juzi kwa familia hizo na Mwenyekiti wa taasisi hiyo tawi la Mwanza, Alhaji Sibtain Meghjee, katika hafla iliyofanyika katika msikiti wa Kisesa Kona Katani humo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi wanyama waliotolewa kwa familia hizo, Alhaji Meghjee, alisema kuwa, msaada huo umetolewa kwa kuzangatia uhalisia wa hali ya maisha ya familia hizo.
Alisema, familia hizo zitaruhusiwa kuuza asimilia 30 ya mifugo hiyo kulingana na jinsi itakavyozaliana, ili kuifanya miradi hiyo iwe endelevu na kubadilisha maisha ya familia hizo ikiwa ni pamoja na kujiinua kiuchumi .
Pia, aliwasistiza wanufaika kuzingatia mkataba,ingawa wanyama hao ni mali yao, lazima wafuate masharti na mwongozo kabla ya kuamua kuuza mifugo hiyo.Aidha, Alhaji Meghjee,alisema kutakuwa na shindano litakalowahusisha familia zilizonufaika wa msaada huo,ambapo mshindi atapata kitita cha sh.500,000.
"Tuliangalia shughuli zinazoweza kufanyika hapa kulingana na mazingira na jiografia, ni ufugaji wa ng'ombe,mbuzi na kuku.Rai yangu kama mtaweza kufuga kisasa,kutakuwa na misaada ya kuinua jamii kiuchumi,"alisema Alhaji Meghjee na kuongeza kuwa, kila familia iliwezeshwa kwa kupata mbuzi wanyama majike (mitamba) manane na mabeberu wawili.
Wakizungumzia msaada huo Salma Maganda ambaye ni mama lishe, alisema ataongeza mtaji kwa ajili ya mendeleo na kuanzisha ujenzi wa nyumba bora, huku Idd Mwehela,akisema,utamsaidia kujiletea maendeleo kiuchumi, kumudu gharma za tiba, kusomesha watoto wake kwa masomo ya elimu ya juu,uwezo ambao hakuwa nao kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kifua.
Mbali na Maganda na Iddi, familia zingine zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na ya Amina Mashauri,Ramadhan Peleka na Ali Shaaban,ambapo Mwenyekiti wa Msikiti huo,wasiwaangushe bali waifanye miradi hiyo iwe endelevu, hatimaye familia zingine nazo zinufaike kwa kupata misaada hiyo.
Msaada kama huo tayari umetolewa na taasisi hiyo ya Bilal Muslim kwa familia mbili za wilayani Muleba mkoani Kagera ambapo kila familia imepata mbuzi kumi.
No comments: