WALIOOKOLEWA KATIKA MACHIMBO YA NYANGARATA KAHAMA KUFANYIWA IBADA.
Na:Shaban Njia, Kahama
VIONGOZI pamoja na Wachimbaji Wadogodogo wa Mgodi wa Shigitwa (SHIGOMICO) Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga umejipanga kuwafanyia Ibada ya kuwaombea Wahanga watano waliofunikwa na kifusi na kukaa kwa siku 41 ndani shimo kabla ya kuokolewa juzi kwa lengo la kuwajenga kiimani.
Mwenyekiti wa bodi ya Mgodi huo uliopo katika Kijiji cha Nyangarata Hamza Tandiko alisema kuwa lengo la kuwasomea Ibada Wahanga hao ni pamoja na kuwajenga kisaikolojia sambamba na kushukuru Mwenyezi mungu kwa kuwaepusha kifo.
Tandiko alisema kuwa kitendo cha Wahanga hao kutoka salama katika tukio hilo sii cha kawaida na kuongeza kuwa wao wameona kutokana na hali walionayo kwa sasa ni bora pia wakawafanyia ibada ya kuwaombea bilaya ya kujali dini walizokuwa kuwa nao.
“Unajua watu hawa kwa sasa bado hali zao sio nzuri na pia katika familia zao tayari misiba ilishafanyika muda mrefu sasa ikiwa ni wengine pia ndugu zao wameisha gawana mali zao kama urithi hali ambayo wakipata fahamu viruzi wanaweza wakahaoji mali zao zilizopo”, Alisema Hamza Tandiko.
Aidha Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa kwa sasa ni vema Watanzania wenye mapenzi mema kujitokeza kuwafariji Wahanga hao ikiwa ni pamoja na kuwasadia katika mambo mbalimbali kwani kwa sasa hawana kitu chochote hali ambayo itawatia moyo na kuwaondolea majonzi walio nayo kwa sasa.
Pia alisema kuwa hapa nchini kuna vyama vingi vya Wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali na kuwataka wasadia wenzao hao kupitia ushirika walio nao ili kuwasaidia katika kupata hata mitaji kwa ajili ya kuanzia maisha hata kama siyo ya uchimbaji kama waliokuwa nayo hapo awali.
Tindiko pia aliiomba Wizara ya Nishati na Madini kukaa na uongozi wa Mgodi wa Nyangalata kuptia chama cha Wachimbaji wadogowadogo Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) ili kuweza kuona kila mmoja atawezaje kuwasaidia watu hao ambao wameathirika kwa kiwango kikubwa.
Katika hatua nyingine iliyojitokeza juzi ni pale Wahanga hao walipohoji matokea ya Uchaguzi wa Uraisi ulifanyika octoba 25 ambapo wao walikuwa tayari wamefukiwa na kifusi hicho kuwa ni nani aliyeibuka mshindi hali ilistaajabisha watu walifurika kuwapa pole katika Hospitali ya Wilaya.
“Hebu tuambiane jamani katika uchaguzi uliopita wa Rais, ni nani aliyeshinda katika Edward Lowassa au Dr, John Pombe Magufuli kwani hatukuwepo katika kipindi hicho si mnajua tulipokuwa jamani, tupeni matokeo halisi na sisi tupate kujua nani aliyeibuka mshindi”. Alihoji Wambura.
Hivi majuzi Wahanga hao wapatao watano waliokolewa na Wenzao katika Machimbo madogomadogo ya Nyangalata Wilayani hapa baada ya kufukiwa na kifusi na kukaa kwa muda wa siku 41 ndani shimo kutoka Octoba tano hadi Mwezi Novemba 14 kabla ya kuokolewa na wenzao.
No comments: