ZAIDI YA FAMILIA 200 WILAYANI ILEMELA ZANUFAIKA NA MRADI WA EAGT LUMALA STUDENT CENTRE.
Judith Ferdinand, Mwanza
FAMILIA 221 katika Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa, zimenufaika na mradi wa kuwahudumia watoto kutoka kaya zenye kipato cha chini, ulioanzishwa kwa ajili ya kuwaendeleza na kuwainua katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa EAGT Lumala Student Centre, Joram Samwel, wakati akizungumza na BMG ofisini kwake.
Samweli alisema, watoto wengi wanashindwa kufikia ndoto zao, kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia, hivyo kupitia kituo chao wameamua kuzisaidia familia hizo, kwa kuwapatia elimu, ujuzi, kuwafundisha ujasiliamali, kuibua vipaji na kuviendeleza, huduma za kiafya na kiroho.
Pia alisema mbali na kuwahudumia watoto na wazazi pia wanapatiwa huduma hasa waliokumbwa na matatizo mbalimbali kama njaa, mafuriko na wale wanaishi na virusi vya ukimwi.
Naye Mchungaji wa kanisa la EAGT Daniel Kulola alisema, tangu kuanza kwa mradi huo familia hizo, zimepata unafuu wa maisha kutokana na kufundishwa ujasiiamali, uzazi wa mpango kwa ajili ya kupata watoto watakaoweza kumudu gharama za kuwahudumia.
Pia alisema, wamewafundisha masuala ya kidini, hivyo wamekuwa na maadili mema, kwani wakifanya jambo kwa kumshirikisha Mungu changamoto za kidunia watazishinda.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii wa kituo hicho Innocent Ivann alisema, wanawafundisha watoto ujuzi mbalimbali kama kushona, uselemala na upishi, ili waweze kujitegemea baadaye endapo watakosa ajira.
Hata hivyo aliiomba, serikali na wadau kuwaunga mkono na kuwasaaidia katika masuala mbalimbali kama kupatiwa eneo la kujenga shule na mabweni ili kuendelea kutoa huduma ya elimu kwa watoto hao.
No comments: