LIVE STREAM ADS

Header Ads

IMEBAINIKA MIRADI YA UJENZI HALMASHAURI YA MSALALA MKOANI SHINYANGA ILIKUWA YA UONGO

Na:Shaban Njia
IMEELEZWA kuwa baadhi ya Miradi ya Maendeleo ikiwa ni pamoja na ile ya Ujenzi wa Barabara pamoja na Vocha za Pembejeo za Ruzuku kutoka Serikalini  iliyokuwa ikifanyika wakati Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala limevunjwa mwaka jana kupisha uchaguzi mkuu ilikuwa imegubikwa na udanganyifu mkubwa.

Mbunge wa Jimbo la Msalala Ezekiel Maige aliyasema hayo juzi wakati wa kikao cha Kawaida cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala kilichofanyika juzi katika ukumbi wa Halmashauri hiyo huku akipinga taarifa ya Kamati ya Ujenzi  iliyokuwa ikisema kuwa ujenzi barabara ulikamilika kwa silimia 100 katika kipindi hicho.

Alisema kuwa kutokana na Mapungufu makubwa ya Taarifa hiyo ya Kamati ya Ujenzi ambayo inaonyesha ilikuwa imejaa uongo Mbunge huyo alishauri Madiwani kuunda kamati kwa ajili ya kufanya uchunguzi pamoja na ukaguzi katika Kata ambazo miradi hiyo ilitakiwa kutekelezwa. 

Aidha alisema kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa juu ya utekelezaji wa miradi ya barababara pamoja na Vocha za Pembejeo za Ruzuku ambazo kwa kiasi kikubwa hazijawafikia Wakulima mpaka kufikia hivi sasa huku taarifa za Halmashauri zikionyesha kuwa kazi hiyo imekwisha fanyika katika maeneo husika.

Aliendelea kusema kuwa karibu kila eneo unalotembelea katika jimboa la Msalala unakutana na matatizo ya Ujenzi pamoja na Vocha hali ambayo wananchi wanakosa imani na uongozi wa wa Halmashauri ya yao husika.

“Tunaomba iundwe Tume ya Madiwani kwa ajili ya kutembelea maeneo husika na wakati utakapofika uamuzi utolewa kuhusu uchunguzi huo katika vikao husika vya Baraza la Madiwani”, Alisema Ezekieli Maige.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Busangi Alexander Mihayo akichangia hoja hiyo alisema kuwa taarifa hiyo ya Utekelezaji ya Kamati ya Ujenzi haiwezi kupokelewa na Madiwani hao kwani ilikuwa haijaandaliwa  vizuri huku ikigubikwa na takwimu za uongo.

Awali katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala, Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Deus Ngeranizya akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashari hiyo Patrick Karangwa alisema kuwa miradi yote iliyotekelezwa katika kipindi ambacho Madiwani walikuwa hawapo kwa mwaka jana ilikamilika kwa asilimia 100 hali ambayo ilipingwa vikali na Madiwani hao.

No comments:

Powered by Blogger.