LIVE STREAM ADS

Header Ads

LEMBELI AMTAKA KAWAWA KUTUMBUA MAJIPU HALMASHAURI YA USHETU.

Na:Shaban Njia
ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Kahama kwa miaka 10 iliyopita kabla ya kugawanyika kuwa majimbo mawili James Lembeli,amempongeza mkuu wa wilaya ya Kahama, kwa kitendo chake cha kuunda kamati  huru, iliyofichua wizi wa fedha zilizotolewa na Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.

Kauli hiyo aliitoa jana na kuongeza kuwa, mkuu huyo wa wilaya Vita Kawawa, anastahili kupongezwa kwa kazi anayoifanya ya kufuatilia matumizi mabaya katika Halmashauri hiyo, ambapo kuna wizi mkubwa uliokuwa ukifanywa na watumishi wakiwemo wakurugenzi ambao wamesababisha kukwama kwa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Kawawa hivi karibuni aliunda kamati ya kuchunguza matumizi ya shilingi zaidi ya bilioni 1 zilizotolewa na mgodi wa Buzwagi na kubaini zaidi ya milioni 800 zimeliwa na watumishi wa halmashauri ya mji kwa kulipa makampuni hewa ya ujenzi fedha hizo na tayari watumishi watano wamesimamishwa kazi akiwemo Mkurugenzi na mhandisi ambao walikuwa wamehamishwa.

Kufuatia hali hiyo Lembeli alisema Kawawa, ameanza vizuri hatua yake ya kutumbua majipu katika Halmashauri hizo, na kumtaka aelekeze nguvu kwa Halmashuri ya ushetu ambapo kuna mamilioni ya fedha yameyeyuka wakati wa ujenzi wa maabara, ambapo mkurugenzi wake Isabela Chilumba amedaiwa kusambaza yeye vifaa vya ujenzi kwa manufaa yake.  

“Nazifahamu Halmashauri zote mbili Ushetu na Kahama kwa kuwa nimekuwa mbunge kwa miaka 10, Kawawa wizi alioukuta Halmashauri ya mji ni mdogo mno ukilinganisha na uliopo Ushetu ambapo baadhi ya madai yamekuwa yakidaiwa, mkurugenzi wake Chilumba kukingiwa kifua na vigogo wa tamisemi hali iliyozolotesha utendaji wa kazi kuanzia ngazi ya Halmashuri, Kata, Kijiji na Kitongoji”, alisema Lembeli.

Lembeli alisema, katika ujenzi huo halmashauri hiyo iliweka pembeni sheria ya manunuzi na kuamua kusambaza vifaa vya ujenzi na mkurugenzi mwenyewe kwa kuchukua fedha kama masurufu na kununua mwenyewe kwa bei aliyoitaka yeye, hali iliyosababisha pesa nyingi kutumika nje ya ujenzi wa maabara hizo

Hata hivyo mkurugenzi Chilumba aling’aka juu ya madai hayo, na kuongeza kuwa Lembeli hapaswi kuzungumzia hayo kwa kuwa kwa sasa sio mbunge wa jimbo hilo, alipaswa kutoa madai hayo wakati akiwa madarakani na kuongeza kuwa hivi sasa hana mda wa kulumbana naye ana muda wa kufanya kazi.

“Sikiliza mwandishi, Lembeli asilumbane na watoto wadogo kama sisi yeye hivi sasa sio mbunge, mbunge wangu kwa sasa ni Elias Kwandikwa alikuwa wapi kuhoji ubatilifu huo alipokuwa madarakani kinachomsumbua ni uelewa mdogo wa sheria ya manunuzi na Halmashauri yangu ndio imeongoza kwa nchi nzima kwa kujenga maabara kwa gharama ndogo,” alisema Chilumba.

Chilumba alisema “nyie waandishi Lembeli awape tu habari za Halmashauri ya Ushetu na mziandike sana mjaze magazeti mimi Lembeli hawezi kunifanya lolote kwa kuwa yuko nje ya uongozi na yeye kama angefanya vizuri kwenye miaka 10 ya ubunge wake asingeshindwa kwenye uchaguzi uliopita, hivi sasa anapaswa akae pembeni”

Katika Madai hayo Chilumba, aliwataka wananchi wampuuze Lembeli madai yake ya kwamba amefuja fedha kwenye ujenzi wa Maabara mwaka jana, ingawa alikiri kwamba ujenzi huo ulifanyika kwa usimamizi wa watumishi wa Halmashauri yake kila Kata ambao walisimamia ununuzi wa vifaa madukani hali ambayo Lembeli alisema ilitioa mwanya wa fedha nyingi kutumika vibaya.

Kabla ya hapo mkuu wa wilaya ya Kahama, aliwaambia waandishi wa habari kwenye kikao chake kwamba, atahakikisha anafuatilia matumizi yote ya fedha zilizotumika vibaya, baada ya kutoka halmashauri ya mji, atakwenda Msalala na baadaye atamalizia Ushetu ambako Lembeli amemtaka kawawa baada ya mji, aende Ushetu kabla ya Msalala kwa madai kuna fedha nyingi zaidi zilizopotea.

Wilaya ya Kahama, ina Halmashauri tatu ambazo  Mji, hulipwa fedha zaidi ya Bilioni 1 na mgodi wa Buzwagi, na Msalala pia hulipwa zaidi ya bilioni moja kutoka mgodi wa Bulyanhulu, huku Ushetu nayo Hulipwa zaidi ya Bilioni 1 na Makampuni ya kununua tumbaku, na fedha hizo hulipwa kila mwaka kama ushuru wa huduma lakini maendeleo ya wananchi yako duni kutokana na matumizi yake kutumiwa vibaya na Halmashauri zote.

No comments:

Powered by Blogger.