LIVE STREAM ADS

Header Ads

NI AIBU KWA SERIKALI YA "HAPA KAZI TU" KUSHINDWA KUAINISHA MPANGO WAKE WA MAENDELEO.

Shughuli ya kwanza ya Serikali baada ya uchaguzi ni kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (kutafsiri ilani yake kwenda kwenye Mpango wa utekelezaji). 

Bunge linapaswa kujadili na kuidhinisha Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kisha Mpango wa mwaka mmoja kuanza kutekeleza Mpango huo wa miaka 5. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) Ibara ya 63(3)(c), Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano hutungiwa sheria kwa ajili ya utekelezaji.

Leo Serikali ya Rais John Magufuli ilipangiwa kuwasilisha Mpango huo wa Maendeleo wa miaka Mitano. Imeshindwa. Imeleta mwelekeo wa Mpango. Haikuleta sheria na Kamati ya Bajeti Imeleta maelezo yake kuhusu Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja ilhali hakuna Mpango wa Miaka Mitano. 

Mwenyekiti wa bunge Andrew Chenge alitaka wabunge wajadili kwa mujibu wa kanuni ya 94 ambayo kimsingi ni Kanuni inayohusu Mpango wa mwaka mmoja. Serikali imejichanganya. Uongozi wa Bunge umechanganyikiwa.

Bunge linapaswa kuagiza Serikali ikalete Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano  ili uidhinishwe na utungiwe Sheria kabla ya kuanza kujadili mipango ya mwaka mmoja mmoja. 

Ni aibu kubwa kwa Serikali ya #HapaKaziTu kushindwa kuleta Bungeni Mpango wake wa Maendeleo wa miaka Mitano na hata ule wa mwaka wake wa kwanza. Itapangaje bajeti zake? Itatekeleza vipi ilani yake? Kuongoza nchi sio kutumbua majipu tu, ni kuendesha nchi.
Zitto Kabwe (Mb)


Kigoma Mjini

No comments:

Powered by Blogger.