LIVE STREAM ADS

Header Ads

RAIA 12 WA NCHI JIRANI WATIWA MBARONI MJINI KAHAMA, SHINYANGA.

Na:Shaban Njia
Kutokana na msako mkali wa siku mbili unaondelea Mkoani Shinyanga uliofanywa na idara ya Uhamiaji, wahamiaji haramu saba raia wa nchini ya Burundi wamekamatwa   huku wengine watano wakichunguzwa  uraia wao.

Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, AnnaMary Yondani aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kufuatia msako wa siku mbili wa kuwatafuta raia wa kigeni wanaoishi nchini kinyume cha sheria.

Yondani alisema kufuatia msako huo Idara yake iliweza kukamata vijana 12 waendesha daradara za Baiskeli na kubaini kati yao 7 ni raia wa Burundi huku wengine watano wakifanyiwa uchunguzi wa uraia wao,wakibainika sio raia wa Tanzania watafikishwa Mahakamani.

“Ndugu Wanahabari na wananchi taarifa ya kazi za misako tulizofanya siku mbili katika Mkoa wa Shinyanga,Wilaya ya Kahama tumekamata vijana 12 na kubaini vijana hao wanaotoka Burundi na wamejikita katika shughuli ya kuendesha Daradar za Baiskeli ambazo hazina kipato hali hiyo inasababisha uharifu kuwa mwingi ndani ya Mkoa wetu,”alisema Yondani.

Alisema vijana hao wamewakamata kwa awamu mbalimbali tofauti ambapo katika msako huo vijana wawili walikimbia na kuzitelekeza baiskeli zao na kuongeza kuwa hadi sasa katika idara ya Uhamiaji wilayani kuna baiskeli 14 za Daradara zimeshikiliwa ambapo 12 zinawahusika na 2 walizikimbia.

Alisema mbali na hilo pia kuna Baiskeli nyingine zipo Idara ya Uhamiaji zimeshikiliwa kutokana na wahusika kubainika ni wahamiaji haramu hivyo walipelekwa Mahakamani na kushtakiwa na baadaye walihukumiwa na kupewa adhabu mbalimbali na baada ya kumaliza adhabu zao waliondolewa nchini.

“Ndugu wanahabari kwetu sisi ni changamoto kubwa kutokana na miundombinu tuliyonazo,tunashindwa kufika vijijini ambako wengi wanakimbilia kutafuta vibarua vya kulima Tumbaku na kazi za mashambani”,alisema Kamishna huyo.

Hata hivyo alisema kuwa mji wa Kahama mkoani shinyanga ndio unaongoza  kwa  kupokea wahamiaji haramu na kusema zoezi la msako litakuwa endelevu na kuwachukulia hatua wale watakaokamatwa wakiwa wameajili raia wa kigeni.

Waliokamatwa katika msako huo ni Mapinduzi Petro,Isham juma,Gozbert Nicodem,Niyonize John,Issa Bernado,Nazar Isengeimana,Sylvester Shimlimana,A Niyokuze,Wizemana Gerlad,Ddon Iman,Musa lazaro,Sospeter Emmanuel pamoja na Twenal Musa Seungu wote waendesha Daradara za Baiskeli Wilaya ya Kahama.

No comments:

Powered by Blogger.