LIVE STREAM ADS

Header Ads

MTUMISHI WA AFYA KATIKA HOSPITALI YA HALMASHAURI YA KAHAMA ATIWA NGUVUNI KWA TUHUMA ZA KUUZA DAWA KWA MFANYABIASHARA.

Na:Shaban Njia
Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, linamshikilia kwa uchunguzi mtumishi mmoja katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama, kwa madai ya kukutwa akiuza dawa na vifaa tiba zenye thamni ya Shilingi 106,000 kwa mfanyabiashara wa duka la madawa kinyume cha taratibu  za utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, Mika Nyange, alimtaja Mtumishi huyo kuwa ni Egbart Kahugya na kwamba alikamatwa akiwa katika mgahawa mmoja mjini Kahama.

Kamanda Nyange alisema mtuhumiwa huyo baada ya kuwekwa chini ya ulinzi ulifanyika upekuzi katika gari yake iliyokuwa kando ya  Mgahawa huo na kukutwa na mzigo huo wa madawa, na kuongeza kuwa Polisi Mjini Kahama, bado inafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo kwa kuwahoji watuhumiwa wote wawili,kabla ya kuwafikisha Mahakamani.

Kwa upande wake Mganga Mkuu katika Hospitali ya Halmahauri ya Mji wa Kahama,Bruno Minja,alishitushwa na kitendo hicho cha Tabibu Kahugya kufanya vitendo vya kibadhirifu ambapo alidai uongozi wa hospitali utachukua hatua stahiki za kimaadili juu ya mtumishi huyo.

Dk.Minja alisema tayari wamechukua hatua za kisheria kwa kufungua kesi kwa tabibu Kahugya,kwa kosa la kupatikana na dawa za serikali kinyume cha sheria kwa kufungua jalada lenye namba KAH/IR/683/2016,baada ya kujiridhisha na kuwaonya vikali watumishi wake wasiowaaminifu,kuondokana na tabia   ya wizi wa madawa na badala yake wafanye kazi kwa uadilifu.  

Aidha alisema baada ya kukamatwa kwa tabibu huyo,kwa kushirikiana na Polisi walifika Hospitalini hapo na mzigo huo na kubaini madawa hayo na vifaa tiba yapo katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni dawa za serikali, la pili  ni dawa halali, na la tatu ni dawa ambazo hazijasajiliwa ambazo usajili wake ulifutwa na mamlaka ya chakula na dawa “TFDA”.

Hata hivyo tukio hilo limedhihirisha kuwa kuna baadhi ya watumishi katika hospitali hiyo si waadirifu na hufanya kazi kwa mazoea,na kujinufaisha binafsi na kusahau maslahi ya Taifa, hali ambayo amedai haikubaliki na kama wataendelea kufanya hivyo wataishia pabaya kutokana na serikali ya sasa kutumia nguvu kubwa kuthibiti wizi wa dawa.

Kufuatia hali hiyo Minja amesema katika serikali ya awamu ya tano lazima watumishi wabadilike kama zamani walikuwa wakiiba sasa basi waache kwa kuwa hivi sasa mikakati iliyopo ni kukomesha wizi wa dawa na vifaa tiba hospitalini,na atahakikisha katika hospitali anayoiongoza vitendo hivyo vinakoma na hatosita kuwachukulia hatua kali watumishi watakaobainika wamefanya ubadhirifu.

No comments:

Powered by Blogger.