BMG INAKUTAKIA SIKUKUU NJEMA YA PASAKA. SOMA HAPA NAMNA BORA YA KUADHIMISHA SIKUKUU HII.
Wewe kama mwana wa Mungu, hupaswi tu kuadhimisha
Pasaka kwa mazoea, bali inakupasa na ni vyema sana kuadhimisha Pasaka kuanzia
moyoni mwako, kwani Mungu anawatafuta watu watakaomwabudu katika roho na
kweli.(Yohana 4:23), hivyo basi, napenda kwa msaada wa Roho Mtakatifu,
tuyatafakari mambo machache kuhusu siku kuu hii ya Pasaka.
HISTORIA YA PASAKA
Katika Biblia, Pasaka ilianza kwa mara ya kwanza
katika kitabu cha Kutoka 12, tafadhali tenga muda ukisome kitabu hiki kizima.
Katika Pasaka hii ya kwanza, wana wa Israel waliagizwa kupakaa damu ya kondoo
kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango yao kabla ya Mungu kuleta pigo la
kumi kwa watu wa Misri, ambalo lilikuwa ni pigo la kuwauwa wazaliwa wote wa
kwanza wa Wamisri.
Mungu aliagiza Wa-Israel wapakae damu hiyo kwenye
milango yao ili Malaika atakapokuwa anapita kuwaua wamisri, asiwaue na WaIsraeli
pia. Na Malaika alipokuwa akipita, aliwaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri, na
aliacha kudhuru kila nyumba ya WaIsraeli, mradi tuu iwe imepakwa damu ya kondoo
mlangoni.
DAMU ILIKUWA YA LAZIMA
Katika Kutoka 12:23, inasema “BWANA apitapo
katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu kwenye vizingiti na kwenye
miimo ya milango naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika
nyumba zetu na kuwapiga ninyi“.
Jambo lililotakiwa hapa ili na Waisraeli
wasipigwe, na wao kuweka damu kwenye milango yao. Bwana alichokuwa anaangalia
si kuona kama nyumba fulani ni ya Muisrael au la, Yeye alikuwa anaangalia kama
kuna damu mlangoni au la. Hii ina maana kuwa kama Mwisrael yeyote asingepakaa
damu ya kondoo huyo katika mlango wake, angeangamia pamoja na Wamisri.
Umeona msisitizo wa damu katika Pasaka hii ya
kwanza? Na siku hiyo ndiyo siku ambayo wazaliwa wa kwanza wa Wamisri walikufa,
na Waisraeli wote wakatoka utumwani Misri na kuanza safari ya kuelekea katika
nchi ya Kaanani waliyoandaliwa na Bwana.
Na baada ya hayo, Mungu aliwaagiza WaIsrael
kuiadhimisha siku hii daima na hata akasema “Watoto wenu watakapowauliza,
‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’,Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka
kwa BWANA, ambaye alipita juu ya nyumba zetu alipowapiga Wamisri“(Kutoka
12:26-27).
Kwa hiyo kuadhimisha Pasaka ni agizo la Mungu.
Na pia Mungu akaendelea kusema “Kwa sababu BWANA aliutenga usiku ule ili
kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri katika usiku huu Waisrael wote wanapaswa
kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimu BWANA katika vizazi vijavyo.” (Kutoka
12:42).
Hivyo ndivyo namna Pasaka ilivyoanza kwa agizo
la Mungu mwenyewe, na ukisoma katika Kutoka 12, ndivyo ilivyoendelea
kuadhimishwa mara nyingi katika kipindi cha Agano la Kale. Kuna wakati wana wa
Israel walikaa muda mrefu sana bila kuadhimisha Pasaka, lakini kila mara
alipoinuka mtu aliyeisoma sheria ya Mungu, walitubu na kuendelea tena
kuadhimisha siku hii ya Pasaka.
Kwa siku ya leo nimeona nikukumbushe namna
Pasaka ilivyoanza ili usiwe unaadhimisha Pasaka kwa namna ya mwili tu, bali
uadhimishe Pasaka kuanzia moyoni. Na ikitokea umeulizwa na mtu asiyeamini au
asiyefahamu, basi uwe tayari kumweleza kwa upole kuhusu Pasaka. Bonyeza HAPA Kusoma Zaidi.
Kwa Msaada wa Mtandao.
No comments: