NI MHIMU KUFANYA YAFUATAYO IKIWA UNAADHIMISHA SIKUKUU YA PASAKA.
Bonyeza HAPA KUSOMA Sehemu ya Kwanza.
YESU KRISTO; PASAKA YETU LEO
Katika Agano la Kale, Pasaka ilianza kwa damu ya
kondoo. Lakini Yesu Kristo alikuja duniani na kujitoa Yeye kuwa Pasaka yetu
badala ya kondoo kama ilivyokuwa hapo zamani katika Agano la Kale. Kwa sasa
tunapoadhimisha Pasaka katika maisha yetu, damu ni muhimu sana, ila sasa siyo
damu ya kondoo, bali ni Damu ya Yesu Kristo.
Yesu Kristo alitupa sisi Damu yake badala ya
Damu ya kondoo. Katika Luka 22 kuanzia mstari wa 7 tuanaona namna Bwana Yesu
alivyosheherekea Pasaka pamoja na wanafunzi wake, tukio ambalo ndiyo lilikuwa
mwanzo kabisa wa meza ya Bwana ambayo huwa tunashiriki leo makanisani na sehemu
mbalimbali.
Katika Pasaka hii, Yesu Kristo aliwapa wanafunzi
wake mkate (kuashiria mwili wake) na divai (kuashiria Damu yake) na akawapa
mkate na kusema “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa
ukumbusho wangu” (Luka 22:19) na pia akawapa divai na kuwaambia “Kikombe hiki
ni Agano Jipya katika Damu Yangu, imwagikayo kwa ajili yenu” (Luka 22:20).
Hivyo basi, tangu wakati huo wa maagizo ya Bwana
Yesu, tunaadhimisha Pasaka kwa kuinywa Damu ya Yesu na kuula mwili wake kama
alivyotuelekeza, na ndiyo maana huwa tunashiriki meza ya Bwana huku tukila
mkate ikiwa ni kama tendo la Imani kuwa tunakula mwili wake Yesu, na kuinywa
divai au mzao wowote wa mzabibi kama tendo la imani kuwa tunainywa Damu ya Yesu
Kristo (Imani bila ya matendo imekufa nafsini mwake).
DAMU YA YESU
Tunapoadhimisha Pasaka,ni jambo la lazima sana
kwamba uitafakari Damu ya Yesu na kuona ni kwanini Yesu aliimwaga Damu yake kwa
ajili yako wewe na mimi. Damu ya Yesu ndiyo mtaji tuliopewa kwa ajili ya
mafanikio yetu ya kila eneo la maisha yetu.
Yesu Kristo alimwaga Damu yake katika matukio
tofauti kwa maana zake tofauti pia:
Yesu alimwaga Damu yake alipotahiriwa kama
ishara ya Damu ya Yesu kuitahiri mioyo yetu, yaani kuifanya mioyo yetu kuifuata
sheria ya Mungu kwa ukamilifu wake wote.
Yesu alimwaga Damu yake ilipotoka kama tone la
jasho alipokuwa akiomba katika bustani ya Gethesmane ili kuvunja ile laana
Mungu aliyomlaani Adamu na kumwambia kuwa “Kwa jasho la uso wako utakula
chakula chako…” (Mwanzo 3:19, Luka 22:44)
Damu ya Yesu ilitoka katika kichwa chake
alipovikwa taji ya miiba, Damu hii ni kwa ajili ya kukomboa namna yetu ya
kufikiri/kufanya maamuzi.
Damu ya Yesu ilitoka katika mkono wake wa
kushoto na kulia, Damu hii ni kwa ajili ya kuibariki na kuleta uhai katika kazi
za mikono yetu.
Damu ya Yesu ilitoka katika moyo wake, Damu hii
ni kwa ajili ya kuleta uzima na uponyaji katika ndoa.
Damu ya Yesu ilitoka katika miguu yake miwili,
Damu hii itaifanya miguu yetu kuwa na shauku ya kwenda kutenda mema, na Damu
hii inatumilikisha kila mahali ambapo nyayo za miguu yetu zitapakanyaga.
Je, ni eneo gani ambalo unataka msaada wa Mungu?
Ichukue Damu ya Yesu na umwombe Mungu juu ya eneo hilo. Unaruhusiwa kunywa Damu
ya Yesu, lakini pia, kwa kadiri ya imani yako, unaweza kupakaa katika sehemu
yoyote ile ya mwili wako au popote ambako unataka msaada wa Damu ya Yesu.
Katika kipindi hiki cha Pasaka, acha mazoea,
bali itafakari Damu ya Yesu na gharama Bwana Yesu aliyoilipa hadi hivi leo
tunapata baraka kwa kuitumia Damu yake.
Soma mistari ya Biblia inayozungumzia tukio zima
la kuteswa,kufa,kufufuka na kupaa kwa Yesu, pia angalia filamu/video
zinazoonesha matukio haya kama vile “The Passion of the Christ” au ile filamu
ya Yesu “JESUS-KISWAHILI” Hivi vitakusaidia sana kuona gharama aliyoilipa Yesu
kwa ajili yako ili ujue namna Yesu Kristo anavyokupenda. Pia nenda Kanisani, na
baada ya ibada pata muda wa kukaa na kutafakari habari hizi za upendo wa Yesu.
TUOMBE…
“Mungu Baba, ninakuja mbele zako kwa Damu ya
Yesu Kristo. Mungu Baba, asante kwa kunipenda kwa kiasi kikubwa namna hii,
maana Neno lako linasema, “Kwa maani jinsi hii Mungu uliupenda ulimwengu, hata
ukamtoa Mwanao wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa
milele”. Bwana Yesu, ninaamini ya kwamba Wewe ni Mwana wa Mungu, na ninaamini
kwamba ulija duniani, ukateswa,ukafa na ukafufuka kwa ajili yangu.
Ninakuomba unisamehe
dhambi zangu zote, na ninakukaribisha katika moyo wangu na maisha yangu yote,
Wewe uwe ndani yangu na mimi niwe ndani yako, na Jina langu uliandike katika
kitabu kile cha Uzima cha Mwanakondoo. Ninaomba Damu yako idhihirike katika
maisha yangu na kunipa uzima ndani yako. Asante Bwana Yesu kwa kunipenda na
kuniokoa, AMEN!!! Damu ya Yesu Kristo ikutunze sasa na hata milele, Amen.
Kwa Msaada wa Mtandao
No comments: