VIONGOZI MWANZA WATAKIWA KUWAJIBIKA ILI KUENDANA NA KASI YA RAIS MAGUFULI.
Judith Ferdinand, Mwanza
Viongozi mbalimbali Mkoani Mwanza wameombwa kumuunga mkono Rais John Magufuli, katika kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, mshikamano, kujituma, kujitoa pamoja na kuwajibika ipasavyo kiutendaji.
Wito huo ulitolewa jana na Diwani wa viti maalum Wilaya ya Ilemela (CCM), Kulthum Abdallah, wakati akizungumza na majira katika ofisi ya kata ya Nyamanoro wilayani hapo.
Abdallah alisema, viongozi wanatakiwa kuwajibika, kushirikiana na kujitoa bila kujali itikadi ya vyama, dini wala kabila, kwa kuhakikisha ahadi walizotoa wakati wa kampeni, wanazitekeleza ili kwenda na kasi ya rais sambamba na kumuunga mkono katika suala la kutumikia wananchi.
Pia alisema, viongozi wanatakiwa kukaa na jamii pamoja na vijana kwa ajili ya kuweka mikakati ya jinsi gani wataweza kujiajiri sambamba na kuwaajiri wengine kwa kutumia mbinu mbalimbali, ili kujikomboa kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi kwa familia na taifa.
Alisema, ni wajibu wa viongozi na wazazi kushirikiana katika suala zima la kuwaelimisha vijana wanaotumia madawa ya kulevya, ili waweze kuacha na kubadilika, kwani itasaidia kuwakomboa kutokana na kupoteza muelekeo wa maisha.
Hata hivyo alisema, watashirikisha wadau mbalimbali sambamba na kutafuta wadhamini, ili kuleta maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wakazi katika kata zilizopo wilayani humo, kwani viongozi na serikali pekee haiwezi.
Vilevile alisema, wameanzisha mabaraza ya watoto pamoja na mtandao wa watoto wanahabari katika kata ya Nyamanoro kupitia Diwani wa kata ya Nyasaka Shabani Maganga, ambao umelenga kugusa wilaya nzima, kwa ajili ya kuwafundisha na kuwaelimisha masuala mbalimbali sambamba na kuoimba halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya mabaraza hayo.
No comments: