LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAADHIMISHO YA VYOMBO VYA HABARI 2016 KUFANYIKA MKOANI MWANZA.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari; Dar es Salaam, Aprili 27, 2016
Wanahabari na wadau wa habari mwaka huu watakutana jijini Mwanza kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD). Maadhimisho hayo yatafanyika katika hoteli ya Malaika Beach Resort jijini humo kuanzia Mei 2 hadi 3, 2016.

Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya mwaka huu ni Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman. Wageni wengine mashuhuri watakaohudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Wasanii, Mhe. Nape Nnauye (mbunge), Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, mh. Alvaro Rodriguez, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) mh. Roeland van de Geer, Mwakilishi Mkazi wa UNESCO Zulmira Rodrigues.

Wengine ni watu mashuhuri mbalimbali kutoka Serikalini, wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania wamethibitisha kushiriki. Wengine ni pamoja na watendaji wa vyombo vya habari, Wabunge, wakuu wa Taasisi za kitaifa zisizo za Kiserikali, Vyuo vya Uandishi wa Habari, wajumbe wa asasi za kiraia, waandishi wa habari wakongwe.

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni tukio kubwa la mwaka kwa vyombo vya habari na kauli mbiu ya mwaka huu ni Kupata taarifa ni haki yako ya msingi: Idai.

Wakati wa maadhimisho haya, tunakumbuka gharama ambayo watu binafsi wanalipa kwa kutoa habari, na kuwakumbuka kwa namna ya pekee watu hao ambao wakati mwingine kwa kutoa kwao habari wanahatarisha maisha yao na kuweka hatarini uhuru wao wenyewe, ili sisi tuweze kupata habari vizuri na kuufahamu ukweli.

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayoadhimishwa Mei 3 kila mwaka duniani kote, ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kusherehekea kanuni za uhuru wa habari na kuwakumbuka wale waliokufa wakati wakijaribu kutekeleza kanuni hizo. Siku hii hutumika kama jukwaa ambalo hutumiwa na wadau wa vyombo vya habari kushinikiza mataifa kutengeneza sheria rafiki za vyombo vya habari zinazoweza huhakikisha uhuru wa habari katika nchi zao.

Maadhimisho ya siku hii kwa mwaka huu wa 2016, yanaadhimishwa sawia na matukio muhimu matatu ya kihistoria:
Maadhimisho ya miaka 250 sheria ya kwanza ya uhuru wa habari duniani, ikijumuisha nchi za sasa za Sweden na Finland.

Maadhimisho ya miaka 25 ya kupitishwa kwa Azimio la Windhoek Azimio la kanuni ya uhuru wa habari.

Mwaka 2016 pia ni mwaka wa kwanza wa mzunguko wa miaka 15 wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Kutokana na hali hii, Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2016 inaonyesha uhusiano kati ya uhuru wa habari, utamaduni wa uwazi na haki ya uhuru wa habari, na maendeleo endelevu katika wakati wa digitali. Jambo muhimu katika haya yote ni jukumu la msingi kwa waandishi wa habari, na umuhimu wa kuwalinda wale ambao huleta huduma hii kwa umma.

Mkutano huo pia utatoa nafasi ya kujadili na kushauriana kuhusu maana ya sheria ambazo serikali imezipitisha na kuwasilishwa kwa mara ya kwanza katika Bunge mwaka jana. Zinajumuisha Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Takwimu, Muswada wa Huduma ya Habari na Sheria ya Upatikanaji wa Habari.

Wakati wa tukio hilo waathirika wa ukiukwaji wa uhuru wa habari watatoa ushuhuda juu ya changamoto walizokabiliana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Taarifa kuhusu ya hali ya vyombo vya habari katika Kusini mwa Afrika iliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika - MISA inayojulikana kama Je Hii ni Demokrasia? itazinduliwa sambamba na Sera ya Jinsia kwa Vyombo Vya Habari vya Jamii.

Maadhimisho haya yanatarajiwa kuhudhuriwa na wadau wasiopungua 250, wa hapa nchini.


Maadhimisho haya yameandaliwa kwa pamoja na MISA-Tanzania, UNESCO, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Umoja wa Mataifa Ofisi ya Tanzania, Taasisi ya Konrad-Adenauer-Stiftung Tanzania (KAS), Chama cha Wamiliki wa Habari Tanzania (MOAT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Klabu ya Waandishi wa Habari Mwanza na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Imetolewa na Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari nchini UTPC

No comments:

Powered by Blogger.