MAKALA: USIYOYAJUA KUHUSU MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR.
Mwalimu
Julius Nyerere (kushoto) na Sheikh Abeid Amani Karume (kulia) wakibadilishana
Hati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili, 1964.
Na
Emmanuel J. Shilatu
Ni miaka 52 imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika
na Wazanzibar liweke historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano
wa Tanzania kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964. Hii ilitokana na ujasiri,
ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na
mahusiano ambayo yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa pande zote mbili
(Tanganyika na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni na kihistoria zilizochangia huu muungano
wetu.
Kutokana na sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika
kabisa kwamba Visiwa vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata
kushikamana kwa pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu
awali tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.
Pia kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya Wakazi
wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi
kushamiri baina yao.
Halikadhalika harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili
tuweze kujitawala wenyewe kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia
kutuunganisha. Inaaminika (na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya
Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa
Mwingereza ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa
kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki
katika mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na asilimia
kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda yake
yalionekana ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa Gombani
Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na ghiliba za
Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili na hatimaye
waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.
Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu
Nyerere ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake zilianza
kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa kuiunganisha Tanganyika
na Zanzibar.
Mnamo April 22, 1964, Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa
zinaunda Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya Tanganyika)
na Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ) walitia sahihi Mkataba
wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano”
(Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni
muungano sahihi kabisa kisheria na unaotambulika Kikatiba.
Siku ya Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi
zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja tu la
kubadilishana “Hati za Muungano”.
Wananchi wa Tanzania walipiga kura kwa mara ya kwanza katika
uchaguzi wa kwanza kabisa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo
mwaka 1965.
Kama nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa
kutiwa sahihi mkataba unaoitwa Hati ya Muungano
(Articles of the Union) na wakuu wa nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere
(Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964 na kuridhiwa na mabunge
ya nchi hizo Aprili 25, 1964 na hatimaye kuwa sheria ya Muungano ya (Acts of
Union) ya mwaka 1964.
Kimsingi sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo
iliyopewa haki ya chombo cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za
Serikali ya Muungano.
Mwanzoni kabisa Hati ya Muungano (Articles of Union) iliyomo
ndani ya sheria ya Muungano iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya
Muungano. Mambo hayo ni kama vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama
(lakini si usalama wa Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za
nchi za nje, utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi wa
fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.
Kwa nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya
Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele kwa
malengo kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule tulioanza
nao awali na halikadhalika maridhiko yanayoendelea kuufanya Muungano huu
uendelee kudumu hadi hii kesho.
Ndio maana mtu timamu
hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea kuboreshwa kila siku (na
itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11 ambapo hii leo yamefikia
takribani 23.
Mengineyo ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama vile;-
Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa za
mafuta na gesi asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti;
utabiri wa hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979;
pamoja na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .
Tusisahau mwaka 1965 iliundwa katiba ya muda ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of The United Republic of
Tanzania) mpaka kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.
Mwaka huo huo wa 1977 (yaani miaka 13 baada ya Muungano
kutokea) kulikuwa na muungano wa vyama vikubwa viwili kuungana kutoka pande
zote mbili (Bara na Visiwani). Vyama hivyo ni TANU (Tanganyika African National
Union) pamoja na ASP (Afro Shiraz Party) cha Zanzibar kuungana na kuunda Chama
cha Mapinduzi (CCM) .
Hatua ama vitendo na mafanikio hayo si tu kwamba yalidumisha
bali hata yaliendeleza kukuza Muungano wetu ambao Jahazi lake liligubikwa na
misukosuko ya mawimbi makubwa baharini uliojaa uzito wa mambo mbalimbali
uliokuja kwa sera ya kero zilizoleta chokochoko mbalimbali katika Muungano
wetu., ambao hatutakiwi kamwe kuusahau maishani mwetu.
Tusisahau mchezo mchafu uliojaa rafu za kutisha uliotaka
kufanywa na Bunge miaka ya 1990 na 1992 ya kutaka kuyakubali madai yaliyotolewa
na kundi la G55 ambalo lilitaka kuundwa
kwa Serikali ya Tanganyika , hali hii ingetuvuruga kwani ilihitaji uwepo na
serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika yatupasa tuzishukuru hekima
na busara za Mwalimu Nyerere kwa kutuokoa na chokochoko ya kero hii.
Pia tusiisahau kero ama chokochoko nyingine ya Muungano wetu
iliyoibuka Decemba 1, 1992, ambayo Zanzibar ilitaka kujiunga na umoja wa Nchi za
Kiislam Duniani (OIC) kama nchi nje ya Muungano.
Tuendelee kukumbuka ni kwa jinsi gani Zanzibar iliyokuwa
inasaka ukuu nje ya Muungano kwa kuibua madai ya Bendera ya Taifa lake
(Zanzibar), wimbo wa Taifa, na nembo yao ya Taifa.
Kwa nyakati tofauti tofauti tumekuwa tukisikia baadhi ya
Wazanzibari walio wachache wakiilalamikia hali nzima ya ongezeko la mambo
kwenye Hati Muungano (Articles of Union) kutoka mambo 11 hadi kufikia 23 ambalo
ni sawa na ongezeko la mambo 12 ambao kwa baadhi yao hawaoni umuhimu wa wa
uwepo wake na hata kutishia kujitoa. Ila asilimia kubwa ya Wazanzibari
wanayaunga mkono, hali iliyo sababisha hoja ya wachache kuzidiwa nguvu.
Pia tumekwisha sikia jinsi gani Wazanzibari wanavyotaka
jambo la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na aina nyingine za
mafuta au bidhaa na gesi asilia iondolewe katika masuala ya Muungano ili
Zanzibar ipate kunufaika zaidi na maliasili zake.
Kukuru kakara za Wazanzibari zinatookana na madai yao ya
kuwa Tanganyika(Bara) imeimeza Zanzibar (Visiwani) katika masuala mazima
yahusuyo Muungano. Ikumbukwe Ubaguzi wa dhana ya Tanganyika umeimeza Zanzibar
si ya kweli na hii imebainishwa katika katiba ya Muungano kuwa kuna Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Haya ni mapenzi ya dhati waliyoonyesha kwa Wazanzibari kwa
kuwaruhusu wawe na serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ikumbukwe Serikali ya
Muungano inaongozwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inaongozwa na Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar na
chombo chao cha kutunga sheria kinaitwa Baraza la Wawakilishi.
Ndugu zangu hali ya kupuuzia na hata kuuchezea Muungano wetu
ni hatari sana tena ni dhambi iliyotukuka. Mathalani Wazanzibari wakiamua
kujiengua kwenye huu Muungano ili wawe kivyao vyao,hawatabaki salama. Mwalimu
Nyerere alishawahi kusema ya kuwa “wakifika kwenye hatua hiyo watagundua kuwa
ndani yao kuna Wazanzibari na Wazanzibara”. Nao wataamua kuwafukuza wale wa
Wazanzibara, lakini hiyo haitakuwa mwisho. Punde si punde watajigundua kuwa nao
(Wazanzibari) wamegawanyika kwani kuna Wapemba na Waunguja, na wakifikia hapo
pia hawatakuwa salama ni lazima machafuko yatatokea.
Daima Wazanzibari watambue ya kuwa dhambi ya kutokutamalaki
kwa dhana ya Unguja na Pemba unatoka na kufunikwa na kivuli cha mwamvuli cha
Muungano. Hivyo umoja, mshikamano, amani na utulivu wao unategemea sana uwepo
wa nguzo hii imara ya Muungano huu tulionao.
Vivyo hivyo kwa watu wa Bara (Tanganyika) ni rahisi kwao
kutafunwa na dhambi ile ile ya ubaguzi watakayo ianzisha nje ya uwepo wa
Muungano ni rahisi sana kwa ukabila, udini, ukanda na hata U-rangi kutamalaki
ndani ya jamii wakishafikia hapo, hawatabaki salama kwani watachafuana tu.
Muungano huu tulionao unawafanya wale wageni, mataifa ya nje
na watu wote wenye hila, donge, roho ya korosho kuogopa kutugusa na kutuvuruga
kutokana na kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina
yetu.
Muungano huu wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa
kusafiri kwa pande zote iwe ni bara ama ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa
mtu wa bara kwenda Visiwani na hata wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi
kwani Uhuru huo wa uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu
tulionao.
Kutokana na uwepo wa uhuru wa kusafiri usio na mipaka baina
yetu, pia Muungano wetu tulionao unazidi kutuongezea fursa na nafasi zaidi ya
uwanja mpana wa ufanyaji biashara. Hali hii imesababisha uwepo wa mzunguko
mkubwa wa pesa ndani yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa zikitoka Visiwani
(Zanzibar) kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya bidhaa kama vile
nafaka, kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.
Pia si jambo geni tena kwa sasa kuona pesa zikivuka Bahari
na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa biashara kama
vile Magari, nazi, Karafuu, Tende na kadhalika.
Muungano huu unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana
tena usio na kikomo wa ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama
kutojulisha au kuwa na upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za
kijamii bora, Muungano hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano sahihi
wa upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya Muungano”
(Articles of union). Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima wa
nyanja za kimaisha yetu.
Ni ukweli uliodhahiri kuwa haitakaa itokee Muungano kama huu
(wa Tanganyika na Zanzibar) hapa Barani Afrika umoja ushirikiano, ushikamano,
amani na utulivu ni sehemu mojawapo ya manufaa ya Muungano huu.
Njia mojawapo ya kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa
kuudumisha Muungano wetu ambao ni urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania
yatupasa tuenzi Muungano wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni
nguzo na fahari ya kipekee na ya aina yake Barani Afrika.
Endapo itatokea kiongozi yeyote Yule ama utawala wowote ule
utakaokuwa na malengo ya kuubomoa ama kuuvunja Muungano huu, basi ajue dhambi
hii itamtafuna yeye na kizazi chake milele.
Mungu atuepushe na mawazo ya kuuvunja Muungano huu vichwani
mwa viongozi/watawala wetu, atuepushe na balaa hili lisijitokeze kwenye Katiba
Mpya ijayo. Kheri ya Miaka 52 ya maadhimisho ya Muungano!!
No comments: