LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHIRIKA LA WADADA CENTRE LAWATAKA WANAFUNZI NCHINI KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA.

Getruda Ntakije na Judith Ferdinand, Mwanza

Wanafunzi nchini wametakiwa kutumia elimu wanayopata ili kubadilisha mitazamo hasi katika jamii  juu ya mila na desturi potofu, inayochangia ongezeko la matendo ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji.


Wito huo ulitolewa juzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Wadada Centre, Winlady Boniface, linalojishughulisha na utoaji elimu juu ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa vijana walioko shuleni na mtaani, katika mahafali ya wanachama ambao ni wahitimu watarajiwa wa kidato cha nne na sita kutoka klabu ya shule ya sekondari ya wasichana Bwiru na Mnarani SFA Wadada Center, yaliyofanyika mkoani hapa.

Boniface alisema, ili kufikia malengo ya kukomesha matendo ya unyanyasaji kijinsia, wasomi wanatakiwa kujitambua, kujiamini sambamba na kutumia elimu wanayoipata kuelimisha jamii, ili iweze kuachana na mila na desturi potofu kama ukeketaji kwa wanawake na kunyimwa fursa katika ngazi mbalimbali za uongozi.

Naye Meneja  wa Mradi wa Kuwezesha Vijana kupitia shirika hilo Christian Noah alisema, wamefanikiwa kuwaelimisha vijana zaidi ya 1000, kutoka kata ya Igombe, Bugongwa na Ilemela ambao wameweza kuripoti na kupaza sauti katika jamii  ili iache kufanya ukatili wa kijinsia.


Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu  wa klabu ya shule ya sekondari ya wasichana Bwiru SFA Wadada Center, Neema Ndebeke alisema, kupitia elimu inayotolewa na  shirika hilo,  limesaidia wanafunzi kujitambua, kujiamini, kujisimamia sambamba na kuwa na uwezo wa kujitetea  wenye  na wanawake wengine wanaonyanyasika katika jamii.

Aidha Mwenyekiti wa klabu ya shule ya sekondari Mnarani SFA Wadada Center Rehema Mathias alilipongeza shirika hilo kuelimisha vijana juu ya ukatili wa kijinsia, kwani kupitia elimu hiyo itakomesha matendo hayo kutokana na jamii kuweza kujitambua.

No comments:

Powered by Blogger.