LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANTRADE KUWAJENGEA UWEZO ZAIDI WAJASIRIAMALI WA MAZAO YA NGOZI.

Judith Ferdinand, Mwanza
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), inatarajia kuendelea kuwajengea uwezo wa uzalishaji, wajasiriamali, ili waweze kutumia fursa zilizopo na kukuza uchumi binafsi na wa Taifa  kupitia sekta ya ngozi.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Tan Trade Edwin Rutageruka,  kwenye sherehe ya kufunga mafunzo ya awali ya utengenezaji viatu vya ngozi kwa wajasiriamali wadogo Kanda ya Ziwa, yaliyofanyika  katika  Chuo cha  Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) tawi la Mwanza kilichopo Ilemela Mkoani Mwanza.

Katika mafunzo hayo, jumla ya washiriki 41 kutoka mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu, Mara, Kagera na Shinyanga walipatiwa mafunzo chini ya ushirikiano wa TanTrade, Sido Mwanza na Chuo cha DIT.

“Sisi kama taasisi tumijipanga kuwajengea uwezo wajasiriamali, waweze kutumia vizuri fursa za biashara zilizopo kupitia sekta  hii muhimu ya ngozi  na hatimaye kuwaongezea kipato  binafsi na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wetu kwa ujumla, ili kufikia malengo ifikapo mwaka 2025 nchi iwe na uchumi wa kati,” alisema Rutageruka.

Pia aliiomba serikali ya mkoa wa Mwanza kupitia manispaa na halmashauri kutenga maeneo yatakayotumiwa na wajasiriamali, kuzalisha bidhaa sambamba na kuwawezesha kuyafikia masoko kwa kupitia fursa mbalimbali  zikiwemo  za maonyesho ya  DITF, Sido Kanda, nanenane na yale ya nje ya nchi yanayoandaliwa na Tana Trade.

Naye Ofisa Elimu Mkoa Hamis Maulid aliyemwakilisha Katibu Tawala Mkoa Kamishina Godwilg Mteve alisema,  matarajio yake kwa washiriki hao, kupitia mafunzo waliopata watatengeneza bidhaa bora zitakazo kubalika katika soko la ndani na nje, hali itakayosaidia  kuleta mabadiliko kiuchumi.

Kwa upande wake Ofisa Mwandamizi wa Tan Trade  Mohamed Mkandara alisema, Mamlaka hiyo imeandaa mafunzo hayo kwa wajasiriamali, waweze kutengeneza bidhaa bora za ngozi zinazokubalika ndani na nje ya nchi, ili kukuza uchumi wa taifa sambamba na kuwaomba wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata kuboresha bidhaa zao.

Hata hivyo Meneja Sido mkoa wa Mwanza Damian Chang’a aliwaomba washiriki hao  kutumia  elimu walioipata, kuendeleza viwanda na kazi zao  pamoja na kupenda bidhaa zinazozalishwa nchini ili kukuza pato la taifa.

Aidha Mkuu wa chuo cha DIT  tawi la Mwanza Albert Mmari alisema, chuo hicho kimetoa mafunzo mbalimbali kama uchakataji wa ngozi, ubunifu, utengenezaji wa viatu na bidhaa za ngozi, uchunaji na utunzaji ngozi, ikiwa ni juhudi za kuongeza thamani ya ngozi sambamba na kutoa ajira kwa vijana.

No comments:

Powered by Blogger.