LIVE STREAM ADS

Header Ads

HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA YAJIPANGA KUJENGA MASOKO.

Judith Ferdinand, Mwanza
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imejipanga  kujenga masoko na kuboresha miundombinu yake katika maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya machinga  kufanyia biashara zao.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Jiji hilo,Adam Mgoyi katika kikao cha baraza la madiwani, kilichofanyika katika halmashauri hiyo.

Hii ni baada ya Diwani wa Kata ya Butimba, John Pambalu, kutaka kufahamu halmashauri hiyo ina mkakati gani wa kuboresha soko la machinga lililopo Mlango mmoja, ili liweze kuwanufaisha wafanyabiashara wengi na kukuza pato katika halmashauri hiyo.

Mgoyi alisema, sheria ndogo za jiji haziruhusu machinga kuzagaa katikati ya mji, hivyo kupitia kikao cha baraza lililopita, waliamua wafanyabiashara hao, kwenda katika maeneo waliopangiwa endapo halmashauri hiyo itaweka mazingira mazuri ya  kufanyia biashara na kuboresha miundo mbinu.

Pia alisema, watashirikisha madiwani wa kata zote zilizopo ndani ya halmashauri hiyo, wakati wa kujenga na  kuboresha miundo mbinu  ya masoko, ili kutatua changamoto za machinga ikiwemo kuzagaa ovyo mitaani.

Aidha alisema halmashauri inamkakati wa muda mrefu wa kuboresha soko la Mlango mmoja kwa kujenga ghorofa moja, ambayo itaweza kuwanufaisha wafanyabiashara wengi na hivyo kuongeza mapato ya halmashauri.

No comments:

Powered by Blogger.