LIVE STREAM ADS

Header Ads

JICHO LA BMG: VIONGOZI WA KIROHO BADILIKENI KULINGANA NA NYAKATI, MAHITAJI NA MAZINGIRA.


Na Kennedy FS
Nawasalimu nyote Katika Jina la aliyehiyari kuwa dhamana ya usalama wa Maisha yetu. Baada ya ukimya mfupi kupisha majukumu mengine, leo ninataka kusema na viongozi wetu wa kiroho hasa Wachungaji na Maaskofu.

Naomba nianze kwa kujenga msingi kwanza.Na ieleweke nia yangu ni njema kabisa. Namna ya zamani ya  kuhubiri Neno la Mungu na sasa ni tofauti sana(sina maana Neno la Mungu limebadilika, Laaa!).
Kwa nini kumekuwa na utofauti huu ninaouona?....Sababu kubwa ni kuongezeka kwa uelewa wa umuhimu wa Neno la Mungu miongoni mwa watu hali iliyochagizwa na Mwingiliano wa watu katika jamii,Changamoto na madhila mengi ya maisha lakini pia wigo wa elimu ya kawaida ya kidunia.
Twendeni taratibu tu mtanielewa. Zamani kuhubiri ilikuwa rahisi sana kwa maana ya ujumbe wa kusema (siyo mazingira ya kufikisha ujumbe). Kwa nini nasema ilikuwa rahisi? Neno la Mungu lilihubiriwa kama KITISHO cha kuwarejesha ama kuwashawishi watu waziache njia zao mbaya na kumgeukia Mungu.
Ndiyo maana ukifuatilia mafundisho mengi ya zamani yalijaa Maonyo na hadithi za jehanamu na kunavyotisha. Yamkini kama umewahi kusikiliza ama kuona  mafundisho ya Nguli na Mwasisi wa Makanisa ya E A G T Mtumishi wa Mungu Hayati .Askofu Moses Kulola, utakuwa unanielewa vizuri.Ulikuwa ukiisikiliza injili yake mpaka mwili unasisimka na kuingiwa na hofu kubwa,nakumbuka hasa lile somo la "Siku Kuu" na mengineyo mengi.
Kwa nini mahubiri ya wakati huo yalikuwa asilimia kubwa yanabeba maudhui ya Maonyo makali na hofu? Na ujumbe wake mara nyingi ulikuwa ni;
OKOKA ACHA DHAMBI,MPE YESU MAISHA YAKO,NJOO KWA YESU N.K.
Sababu ni hii hapa; Zamani watu kwa sababu ya giza la kiuelewa , walilichukulia suala la kumcha Mungu kama swala la ziada. Wengi walimpa Mungu nafasi ya mwisho kabisa , na hata walipoenda makanisani walienda kama desturi tu lakini hasa si kwa kunuia kumanisha kujiunganisha na Mungu.
Ndiyo maana ilikuwa ni kawaida sana hata waliojiita waumini wa imani ya Kristo, Tegemeo lao la msaada katika mambo yaliyoonekana kuwa juu ya uwezo wao kuwa Waganga wa Kienyeji nje kabisa na misingi ya imani yao ya Kikristo. (Naomba ieleweke kuwa si waumini wote na wala sina nia ya kuondoa uhalali wa waganga wa kienyeji kama wapo kihalali).
MAMBO YAMEBADILIKA KABISA NDUGU ZANGU VIONGOZI WANGU WA KIROHO.
Siku hizi waumini wanataka kufundishwa habari za;
-Mambo ya fedha na uchumi
-Biashara
-Uongozi
-Siasa
-Ujasiria Mali
-Mahusiano n.k.n.k.
Leo hii ni lazima wachungaji wetu na maaskofu n.k wafundishe Neno la Mungu katika maeneo yote na tena kwa ustadi na ubunifu mkubwa kwa kuyahusanisha hali halisi ya Maisha ya sasa na kuyatolea majawabu kutoka kwenye Biblia kwa kuwa ni ukweli kwamba Biblia ni kila kitu na inayo majawabu ya kila kitu.

ANGALIZO:
Sina maana kwamba sasa mahubiri ya kuonya na vitisho ama ujumbe wa kuokoka usihubiriwe...laaa!! Ila namna ya kuhubiri iwe ya weledi na ubunifu zaidi kutegemeana na mazingira ya wakati wa sasa.
Leo katika makanisa yetu kuna wasomi,matajiri,wafanyakazi, maskini n.k.tofauti kabisa na fikra za zamani kwamba makanisani walipaswa kwenda hohehahe.
ANGALIZO
sina maana ya kwamba wasomi ,matajiri ,wafanyakazi wako juu ya Neno la Mungu ,HAPANA...
Lakini wanapokuja kanisani wanakuwa na changamoto za kazi zao,biashara zao, mahusiano yao, masomo yao n.k
Hivyo lazima Neno likifundishwa litoe majawabu katika changamoto zao hizo.
KWA MFANO:
Neno lisiishie kuhubiri utakatifu kila siku , lazima pia Watumishi wa Mungu wabainishe sababu zinazosababisha waumini wao kushindwa kutunza utakatifu huo.
Natoa mfano, Kwa mfano mtu ambaye hali yake kiuchumi ni mbaya ana msongo wa atakula nini n.k ni ngumu sana kutunza utakatifu wake.
Mfano2.
Watumishi wasiishie kufundisha imani wakaishia hapo na kuwaaminisha waumini kuwa hodari wa imani na kwamba kila kitu kitakuja kwa imani ....hapana....lazima waende mbali zaidi kuwaeleze kwamba imani ya kweli ni ile inayoambatana na matendo...
Waandae masomo ya biashara,mafanikio kibiblia na kuyafundisha kwa waumini wao.
Nasemahaya kwa sababu nina ushuda wa watu waliaminishwa vibaya , wakawa wanashinda kanisani siku saba za juma bila kufanya shughuli yoyote ilhali wakiamini kwamba yamkini siku moja wangefanikiwa.....Iliwagharimu sana mpaka walipoamua kuiweka imani hiyo katika matendo.
NGOJA NISEME KERO NYINGINE INAYOCHANGIA MAKANISA MENGI HASA YA KILOKOLE KUKOSA WASHIRIKA AMA KUWA NA WASHIRIKA WA AINA MOJA TUU.
Matumizi ya Muda na udhibiti wa Muda. Kama nilivyosema huko juu , kwamba mambo yamebadilika sasa si kama zamani,licha ya ukweli kwamba sasa hivi uelewa wa watu kumcha Mungu wakiwemo wasomi,Viongozi,Wafanyakazi n.klakini changamoto za maisha na ugumu wa maisha unaosababisha watu kuwa na majukumu mengi nao umeongezeka.
Wachungaji wetu lazima walifahamu hilo na wawe wabunifu wa kuzingatia muda katika mahubiri yao.
HAIWEZEKANI...mtu awe kanisani tanngu saa 1,2,3-7,8,9 na wengine mpaka jioni ,hiyo ni jumapili pekee bado siku za juma...
Utake usitake hao washirika niliowataja hapo juu utawapoteza
tu...
Haiingii akilini ,kwamba wakati huohuo unawafundisha umuhimu na faida ya kutoa sadaka ikiwemo ya Fungu la kumi lakini wakati huohuo hauwapi nafasi ya kwenda kuwajibika ili wapate hizo sad aka!!!
NAOMBA NIWAPE USHUHUDA HUU WA KWELI NILIOUSHUHUDIA MWENYEWE.
Fuatilia utalusaidia. Miaka michache iliyopita nilikuwa sehemu ya mshirika mwasisi wa huduma moja katika mkoa mmoja. Baada ya huduma kuanza, mikakati mbali mbali ya kimavuno ya washirika tuliiweka na maramoja tukaanza kuifanyia kazi.
Tukaanza kuwapata washirika wa aina zote wakiwemo wafanya kazi,wanafunzi wa vyuo,wafanyabiashara na watu wa kawaida tu wa pale mtaani ambao wengi wao walikuwa na muda mwingi wa kuwa nyumbani. Siku chache baada ya washirika wa makundi Yale ya nje na wale wa mtaani wakawa hawaji tena jumapili wala siku za kawaida.
Kama ilivyokawaida yetu walokole , tukaanza kumuita Bwana katika hili aingilie kati pamoja na kuunda jopo la kuwafuatilia majumbani kwao kujua sababu. Taarifa za jumla za hao washirika zikawa ni zile za kiulokolelokole;
-Tuko pamoja pastor
-Mbarikiwe
-Tutakuja
Siku zikaendelea kusongea bila kuwaona licha ya kutia moyo katika majibu yao. Wengine wakawa wanatoa sababu kivuli, huko mbali sana...Kwa kuwa nami nilikuwa kiongozi na Moja kati ya waliokuwa wanashiriki kuwafuatilia ,nikaamua kukaa chini kujiuliza kwa nini tumewapoteza kundi lile la washirika?
HAYA NDIYO MAJIBU YANGU NILIYOYABAINI:
1.Ibaada kuendeshwa kwa muda mrefu huku kukiwa na ratiba nyingi zisizokuwa za lazima katika ya ibaada. Nilibaini kwamba ibada hasa za jumapili zilikuwa zinachukua hadi masaa 7 mpaka 9 kwa waimbaji na wanamaombi.Kisha baada ya hapo ratiba ya vikao kwa baadhi ya watu wakati mwingine washirika wote ...hali hiyo ilisababisha madhila kwa waliowengi na kushindwa kudumu nasi
 2.Uwepo wa ratiba nyingi siku za juma. Licha ya kwamba
kanisa lilikuwa mbali lakini bado kulikuwa na ratiba nyingi siku za wiki, wanafunzi wa vyuo walilalamika kushindwa kukutanisha ratiba zao zikiwemo majaribio na majadiliano n.k hivyo nao tuliwapoteza.
Sababu nyingine haipendezi kuisema hapa na ambayo pia sikuweza kumshauri mchungaji kwa kuhofia kuingilia maelekezo ya Roho wa Bwana kwa Mchungaji.
LAKINI HII YA MUDA...Nashukuru niliweza kumshauri kwa kina mchungaji na angalau mpaka natoka katika mkoa huo , Masaa ya ibada yalikuwa chini ya masaa matano. Kwa kuanzia. Viongozi wangu mbadilike,Muda mzingatie na ujumbe utosheleze mahitaji ya changamoto za sasa, vinginevyo washirika wataendelea kumiminika katika makanisa ya Vipaumbele vya miujiza na siyo kuifundisha miujiza ya kweli iliyopo katika Neno.
Miujiza mingine bandia kama simu bandia,Yesu katika kuponya kwake hakuwa na kanuni maalumu ,wengine aliwaponya kwa maneno tu,wengine hivi, wengine kwa njia ile n.k..
ANGALIZO. Sina maana ya kwamba miujiza na ufunuo kwa sasa havipo....Laa!

No comments:

Powered by Blogger.