LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAMLAKA YA MAENDELEO YA BIASHARA TANZANIA YAJIANDAA KUSHIRIKI MAONYESHO YA NANENANE MWAKA HUU.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Na Judith Ferdinand, Mwanza
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TAN TRADE),  imejiandaa kushiriki  ipasavyo kwenye sherehe za maonyesho ya nanenane mwaka huu, katika mikoa  mitano ikiwemo Lindi, Mwanza, Arusha,Morogoro na Mbeya.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tan Trade, Edwin Rutageruka, wakati akizungumzia maandalizi ya maonyesho hayo na kuongeza kwamba, maonyesho hayo  yatasaidia mamlaka hiyo, kuwatambua wafanyabiashara na wajasirimali wenye uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye kukubalika katika soko la ndani na nje.

Pia alisema, itasaidia kupata viwanja kwa ajili ya kufanikisha malengo ya mamlaka hiyo ya  kuwa na maonyesho endelevu katika kanda mbalimbali  nchini pamoja  na kupanua wigo wa kibiashara kupitia  fursa hizo, ikiwemo ya sabasaba kuacha kuishia tu mkoa wa Dar es salaam.

Hata hivyo alisema mamlaka hiyo ikishirikiana na wadau mbalimbali, itahakikisha ndani ya uwanja mmoja  wanajenga kumbi za kisasa kwa ajili ya maonyesho, miundombinu ya mikutano pamoja na hoteli yenye hadhi ya nyota 3 au 4, ili kuongeza ajira na uchumi wa nchi.

Alitanabaisha kwamba kupitia maonyesho hayo, wananchi watapata fursa ya kujua majukumu ya mamlaka hiyo juu ya ushauri wa fedha na taarifa za biashara kwa serikali sambamba na kuona bidhaa zinazozalishwa nchini.

Vilevile aliwaomba wananchi kubadilika na kupenda bidhaa za ndani,kwani taifa lililoendelea linatokana na soko la ndani kwa jamii kuunga mkono bidhaa zao.

"Tupende bidhaa zetu zinazozalishwa hapa nchini kama Hayati Rais Karume alivyosema Kipende chako hadi usahau cha mwenzio, ambapo huo ndio msemo sisi kama mamlaka tunauendeleza ili kuhakikisha watanzania wanapenda bidhaa zao". Alisema Rutageruka.

No comments:

Powered by Blogger.