LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAWEKEZAJI KUTOKA NCHINI KOREA WAFIKA JIJINI MWANZA KUSAKA FURSA ZA UWEKEZAJI.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Judith Ferdinand, Mwanza.
Wawekezaji kutoka nchini  Korea Kusini wametembelea Mkoa wa Mwanza katika manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kutafuta maeneo ya uwekezaji.

Wakorea hao wamefika mkoani hapa ikiwa ni matunda ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angelina Mabula, alipotembelea nchini Korea Kusini mapema Juni 2016 ikiwa ni jitihada za kufungua milango ya Maendeleo kwa Wilaya ya Ilemela na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.

Akizungumza juzi  kwenye kikao kifupi cha mkakati wa uwekezaji katika Mkoa wa Mwanza, Meneja msaidizi wa Strategic Operation Team, Alex Gang alisema endapo watapa eneo la uwekezaji wanaahidi kumiraisha mahusiano watakayoyaanzisha,na yenye  tija kwa pande zote mbili.

“Tumetembelea maeneo mbalimbali kuona ni fursa zipi zinaweza kuwekezwa katika mkoa huu, baada ya kujiridhisha tunawaahidi  kuimarisha mahusiano tuliyoyaanzisha ili yaweze kuwa na tija,”alisema Gang.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella aliwakaribisha wawekezaji hao na kuwaeleza fursa mbalimbali zinazopatikana katika mkoa huo, zikiwemo uvuvi, kilimo, ufugaji, michezo na biashara.

Pia aliwahakikishia kuwepo kwa maeneo makubwa ya kujenga viwanda ambayo hayatakuwa na  migogoro.

“Tuna maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji, mfano lipo eneo lililopo Nyamong’horo linafaa kwa kujenga viwanda,  pia zipo fursa nyingi za kibiashara kuanzia sekta ya kilimo cha pamba, uvuvi, na ufugaji, sekta hizi zikitumiwa vizuri zinaweza kuleta tija kwa taifa letu,”alisema Mongella.

Mongella alisema, mkoa wa Mwanza ndio kiini cha nchi za Afrika Mashariki  katika soko na biashara ambapo bidhaa zinazozalishwa katika mkoa huo  zinawafikia watu hao kwa urahisi,vilevile  ni mkoa wa pili ukitanguliwa na jiji la Dar es Salaam katika uchangiaji wa  uchumi kitaifa.

“Bado tunaruhusu wawekezaji wengi kutoka nchi mbalimbali kufika katika mkoa wetu, kwani zipo fursa nyingi na  nitakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha wanapata sehemu nzuri za kuwekeza,”alisema

Kwa upande wake Mbunge wa Ilemela Angelina Mabula alisema, kupitia wawekezaji hawa wananchi watapata ajira, miundombinu itaimarika sanjari na kuboresha maisha yao kunakochochewa na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

Mabula alisema kama  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi atahakikisha  wanaepusha migogoro ya kiuwekezaji inayotokea mara kwa mara kati ya wananchi na wawekezaji.

“Ombi langu kwa wananchi wafungue njia na wawe tayari kupokea ugeni huu, kwani tuliposema serikali ya awamu ya tano ni viwanda hatukubahatisha, na kwamba fursa zimeanza kujitokeza, hivyo wafungue milango kwa ajili ya kuzipokea,”alisema Mabula.

Edmond Joseph mkazi wa  Jiji la Mwanza walipongeza ujio wa wageni hao na kuiomba Serikali kuwaruhusu kuwekeza mkoani Mwanza ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana.

No comments:

Powered by Blogger.