LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAZIRI WA VIWANDA ATAKA UTAFITI UFANYIKE ILI KUJUA MAENDELEO YA VIWANDA VIDOGO VIDOGO NCHINI.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Na James Salvatory, BMG Dar
Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, Dkt.Charles Mwijage, ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushrikiana na wadau wa maendeleo nchini ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Viwanda Duniani (UNIDO) na Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) kuendelea kufanya utafiti ili kubaini idadi na maendeleo ya viwanda vidogo vidogo.

Ametoa kauli hiyo jana Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya uzalishaji bidhaa viwandani mwaka 2013.

Mwijage alisema katika mataifa yanayoendelea duniani ikiwemo Korea Kusini, Malaysia na Singapore uchumi wa nchi hizo umeweza kukua kwa kiwango kwa juu zaidi kutokana na kuweka mkazo katika kuendeleza viwanda vidogo na vya kati.

Alisema katika kuharakisha kasi ya maendeleo ya viwanda  vidogo vinavyopatikana nchini, wizara yake imekusudia kuwajengea hamasa watanzania kupendelea kujenga viwanda vidogo vidogo na vya kati, kwani kukua kwa sekta ya viwanda nchini kutaisaidia kuinua uchumi wa nchi.

“Asilimia 25 hadi 40 ya mazao ya kilimo yanayovunwa huharibika kabla ya kufikishwa kiwandani, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imekusudia kujenga viwanda vidogo vidogo ili kuwawezesha wakulima wapate sehemu nzuri zaidi za kuhifadhi mazao yao,” alisema Mwijage

Naye Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt.Albina Chuwa, alisema kuwa matokeo hayo yanaonyesha mafanikio katika sekta ya viwanda ikiwemo kuongezeka kwa ajira zipatazo 264,223 nchini na kuchangia uchumi kwa takribani Shilingi bilioni 8.0 kwa mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.