LIVE STREAM ADS

Header Ads

WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU JIJINI MWANZA WATOA KILIO CHAO.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

 Judith Ferdinand, Mwanza
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu jijini Mwanza wameiomba  serikali,wadau,wafadhili na jamii kwa ujumla, kuwapa kipaumbele,kuwalinda,kuwasikiliza na kuwasaidia.

Ikumbukwe kuwa yapo madhara makubwa, tukiacha  jamii iwe na watoto wanaoishi mtaani na endapo hali hii ikiendelea kukua taifa la baadaye na ulimwengu vitakua hatarini.

Hayo yalisemwa jana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika maadhimisho ya  siku ya Watoto wanaoishi mtaani duniani,yenye kauli mbiu "Mtujali watoto tunaoishi mtaani,huu ni muda wetu" yaliyofanyika  kwenye uwanja wa Furahisha mkoani Mwanza, nakuandaliwa na Shirika la Railway Children Afrika nchini Tanzania na kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mmoja wa watoto walioashiriki katika maadhimisho hayo Vumilia Mlasa alisema,wao ni watoto kama wengine,wanaitaji kusikilizwa,kupendwa na kupatiwa mahitaji,hivyo wanaiomba serikali,jamii na wafadhili kuwasaidia ili kufikia malengo yao.

"Sisi watoto tuliopo katika mazingira magumu, tunaomba wadau kwa ujumla,muendelee kutusaidia,tuchukulieni kama ndugu na rafiki,tupendeni,mtuthamini,tulindeni,mtujali,tuleeni vema pamoja na kutupatia elimu," alisema Mlasa.

Kwa upande wake Emmanuel John alisema, wanaimani wadau wakiwajibika ipasavyo,itawasaidia siku za usoni kuwa watu wema sambamba na kuwaomba wazazi na walezi kuhakikisha familia ni mahali salama pa kuishi,jambo litakalosaidia kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Mwanza Wambura Kizito ambaye ndiye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, aliwaomba wadau kuendelea kushirikiana na serikali kusaidia watoto hao sambamba na wazazi na jamii kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake,ili kumaliza tatizo la watoto wa mtaani na kuwa na taifa bora baadae.

Hata hivyo Meneja Mradi wa  Railway Children Africa Aneth Isaya alisema, mpaka sasa shirika hilo linahudumia zaidi ya watoto 200,licha ya kukumbana na changamoto kutoka kwa watoto hao,ambao wamekuwa wakitoa taarifa za uongo za mahali walipotoka na jina,ikiwa ni jitihada za kuwarudisha kwao.

Isaya alisema, kumekuwa na ongezeko la watoto wa mitaani ukilinganisha na miaka iliyopita,ambapo chanzo ikiwa ni familia wazazi kukosa upendo, kutowasikiliza wanachohitaji pamoja na hali ngumu ya maisha.

Pia aliiomba,serikali iwasaidie kuwa na mfumo rahisi utakaotumika wakati wa kuwarudisha  nyumbani kwao pamoja na kujitoa na kuunga mkono kundi hilo moja kwa moja kama ilivyo kwa watoto wengine.


No comments:

Powered by Blogger.