LIVE STREAM ADS

Header Ads

MABATINI STARS YATOA KICHAPO KIKALI NDONDO CUP JIJINI MWANZA

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.

Judith Ferdinand, Mwanza
Timu ya Mabatini Stars imeilaza chali timu ya Igoma Heroes  kwa kufunga goli 6-3, katika mashindano ya Ndondo Cup yanayoendelea kutimua vumbi katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Katika mchezo huo uliochezwa jana na kukutanisha timu hizo kutoka kundi B, ambapo kipindi cha kwanza  Igoma Heroes  walianza mashambulizi kwa kasi ambayo yalizaa matunda na dakika ya 7 walifunga goli la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake Bosco Kakoko.

Mabatini Stars walisawazisha goli kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji wake Frank Kulwa dakika ya 17 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kanichi Andrew ambaye alifanikiwa kuongeza goli la pili dakika ya 26 huku  Noel Mwaya akifunga goli la tatu.
Katika kipindi cha pili Mabatini Stars iliendeleza mashambulizi  na kufanikiwa kuongeza magoli  matatu ambayo yalifungwa na washambuliaji wake Frank kulwa aliyefunga magoli 2 dakika ya  57 na  77 huku  Julius John akifunga dakika ya 79, ambapo wapinzani wao  Igoma Heroes walifanikiwa kufunga magoli mawili kupitia kwa  Michael Mbigo dakika ya 81 na Bosco Kakoko dakika ya 90.

Frank Kulwa ndio aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo,mara baada ya kufunga magoli matatu, na kupatiwa zawadi ya  shilingi 30000 kutoka kwa HASFU Barber Shop.

Kulwa alisema, amefanya vizuri kutokana  na maandalizi,kujituma pamoja na umakini,hivyo ataendelea kufanya vizuri na kuwaomba mashabiki wa timu hiyo kuja uwanjani kuwaunga mkono na kuwatia moyo wachezaji.

Naye Bosco Kakoko alisema, mazoezi ndio jambo la msingi licha ya kupoteza mchezo wanajipanga na mechi ijayo na anaimani watafanya vizuri.

Hata hivyo katika mchezo huo kipindi cha pili wachezaji wa Igoma Heroes Joachim Dickson na,Joseph Katana walipewa kadi nyekundu  baada ya kuwafanyia madhambi wachezaji wa Mabatini Stars  Noel Mwaya na Macha Mshanga.
Wakati huo huo  katika mechi iliyochezwa mchana  na   kukutanisha timu  kutoka kundi A , timu ya Mnadani Fc iliichapa VIVA FC goli  2-0.

Mnadani FC ilifunga magoli hayo kupitia kwa washambuliaji wake Baraka David dakika ya 30 na Johanea Andrea dakika ya 54.

Aidha katika mchezo huo Baraka David ndie aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo na kupatiwa zawadi ya shilingi 30000.

No comments:

Powered by Blogger.