LIVE STREAM ADS

Header Ads

Makala: Ukosefu wa huduma bora za afya vijijini, huchangia vifo vya akina mama na watoto Tanzania

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.

Sesilia Peter (kulia) mkazi wa kijiji cha Jinjimili wilayani Magu, akizungumza na mwandishi wa makala hii siku tatu baada ya kujifungulia njiani akielekea kituoni kutokana na kutokua na huduma za afya karibu.
Na Blandina Aristides, Mwanza
Miongoni mwa Matatizo makubwa yanayoikabili Tanzania ni pamoja na  vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutokana na matatizo ya uzazi.

Lengo la tatu katika malengo endelevu ya kidunia, yamelenga Kupunguza vifo vya mama wajawazito chini ya 398 kati ya 100,000 kila mwaka ,hii itafanikiwa zaidi endapo kutakuwepo na huduma bora za afya hususani maeneo ya vijijini.

Juni 20 mwaka 2016, Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr. Mpoki M. Ulisubisya, alitoa hotuba yake  katika uzinduzi wa matokeo muhimu ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto pamoja na Malaria nchini Tanzania kwa Mwaka 2015-2016 (TDHS- MIS) ambapo alieleza mambo mbalimbali juu ya afya ya uzazi.

Alieleza kuwa Sekta ya Afya ni miongoni mwa Sekta muhimu sana kwenye jamii  katika kuchangia uboreshaji wa uchumi wa Nchi na kupunguza Umaskini na kwamba kukiwa na taarifa sahihi za afya za Wananchi, ni fursa ya pekee ya kuboresha na kuimarisha ustawi wa uchumi wa Taifa.

Alifafanua kuwa, Serikali imefanya juhudi katika  kuhakikisha  lengo hilo linafikiwa ambapo vifo vya  watoto wachanga, chini ya mwaka mmoja vimepungua  kutoka vifo 51 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai katika Utafiti wa mwaka 2010 kufikia vifo 43 mwaka 2015/16 lakini pia vimeendelea  kupungua  kutoka vifo 81 mwaka 2010 na kufikia vifo 67 mwaka 2015.

Pamoja na kushuka kwa vifo hivyo, bado kunauwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa idadi ya vifo vya  mama na mtoto kutokana na kutokuwepo kwa huduma bora za afya  vijijini.

Ukosefu wa huduma bora za afya katika kijiji cha Jinjimili wilayani Magu mkoani Mwanza ni moja ya kichocheo cha kuwepo kwa ongezeko la Vifo vya mama na mtoto lakini  pia huchangia kuwepo kwa magonjwa ya kuambukizwa na yasiyo ya kuambukizwa.

Hali hiyo inatokana na kutokuwepo kwa  zahanati pia vituo vya huduma  za afya vilivyo karibu katika  kijiji hicho lakini pia hata katika  baadhi ya vijiji na kata za wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Zaidi ya wanawake 302 walijifungulia nyumbani na baadhi yao njiani kwa kipindi cha  mwaka mmoja  bila kuwa na usimamizi kutoka kwa wahudumu wa afya lakini pia wanawake hao hukabiliwa na matatizo ya maradhi ikiwemo vifo vya watoto na kina mama,uchunguzi umebaini.

Kutokana na tatizo hilo, kumekuwa na maradhi mbalimbali ambayo yamekua yakiwaandama wanawake wanaojifungua wakiwa nyumbani ikiwa ni pamoja na kutokwa damu nyingi nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha cha mimba, anemia (upungufu wa damu), maralia kali na fistula.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kituo cha afya cha kabila zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 25 wanawake vijijini hawana uelewa wa ubora wa huduma za hospitali na  madhara ya kujifungua nyumbani ama njiani bila kuwa na msaada kutoka kwa wataalamu wa afya ya uzazi.

Pamoja na kutokuwa na uelewa katika hilo, bado wananchi wa vijiji vyta jinjimili hawana huduma bora za afya  jambo linalochangia kuwepo kwa wimbi kubwa la matatizo ya uzazi kwa akina mama lakini pia kuwa chanzo kikubwa cha kusababisha vifo visivyo tarajiwa.

Kutokuwepo kwa Zahanati katika Kijiji hicho, kumewafanya wanawake kuwa na destuli ya kujifungua wakiwa nyumbani, na wakati mwingine hujifungulia njia kutokana na umbali uliopowa zaidi ya kilometa 8 kutoka kijiji kwenda kwenye kituo cha afya Kabila.

Lakini pia kumesababisha wakina mama waliowengi kutohudhulia kliniki wakati wa ujauzito jambo ambalo ni hatari kwa afya na hatimaye kuchangia  kuwepo kwa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha Ukimwi kwa namna moja ama nyingine.

Takwimu kutoka hospitali ya wilaya ya Magu zinaonesha kuwa wanawake  150 kwa kipindi cha  Julai 2016 hadi Julai 2017, wamebainika kuwa na maambukizi ya V.V.U kati ya wanawake  2458 walio anza kliniki hospitalini hapo huku 74 walijikuta na maambukizi baada ya kupima.

Katika malengo endelevu ya kidunia, lengo la tatu  kipengele cha nne kinaeleza  juu ya kutokomeza maambukizi ya UKIMWI, kifua kikuu, na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kama vile malaria, kisukari, shinikizo la damu, vikope, nimonia, na magonjwa yatokanayo na maji.

Makusudi ya lengo hilo ni  kuhakikisha afya njema na ustawi kwa watu wa rika zote unaongezeka ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kuishi maisha yenye afya bora na kuongeza umri wa kuishi  ifikapo mwaka 2030.

Aidha, itawezekana vipi ikiwa wananchi wa vijijini wataendeleza destuli ya kujifungua wakiwa nyumbani lakini pia kama huduma za afya hazitapelekwa karibu kama sera ya afya ya mwaka 2007 inavyoeleza.

Pamoja na kuwa lengo hilo, linazitaka serikali za mitaa  kupunguza vifo vya mama wajawazito hadi chini ya 398 kati ya 100,000 wanaojifungua kila mwaka nah ii itawezaka endapo huduma hizo zitapelekwa vijijini.

Mtazamo wa kidunia unalenga kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na walio chini ya miaka 5 viwe vifo 51 kwa vizazi hai 1,000 kwa watoto wa kiume na vifo 41 kwa vizazi hai 1,000 kwa watoto wa kike.

Shirika lisilo la kiserikali la Evidence For Action (E4A) Tanzania linaeleza kuwa, Wanawake 8,500 hufariki dunia wakati wa ujauzito au kwa matatizo ya uzazi kila mwaka nchini.

Kwa mujibu wa  Mkurugenzi wa shirika hilo Tanzania, Craig John Felar  anaeleza watoto wachanga 50,000 hufariki dunia ndani ya mwezi wa kwanza baada ya kuzaliwa na kwamba kwa mwaka Tanzania,inapoteza wakazi wote  wa vijiji 20 kama wakazi wake wanakuwa zaidi ya 13,00.

Marko Samweli,Ni muuguzi katika Kituo cha Afya cha Kabila wilayani Magu ambaye ameeleza kuwa wanawake  wanao jifungua nyumbani ama njiani kwa wakati huo, wanaweza wasiwe na tatizo.

Pia anafafanua kuwa, wanawake walio wengi wanapobaini hali ya afya zao  kuwa mbaya baada ya kukaa muda mrefu akiwa amejifungua, ndipo hukimbilia katika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu  matokeo yake tatizo linakuwa kubwa kwani anakuwa amekaa nalo muda mrefu bila yeye kujua.

 “Mama yeyote anapojifungua bila kuwa na huduma bora za kiafya kwa wakati huo hawezi kuona tatizo, bali linakuja baadae na wakati huo limeshakua kubwa kiasi cha kusababisha kifo au kukomaa kwa ugonjwa.”alisema Marko.

Kaimu mratibu wa huduma ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Magu, Norah Joseph anaeleza kuwa, miongoni mwa madhara yanayowakabili wanawake waliojifungulia nyumbani na watoto ni pamoja na anemia, kifafa cha mimba, maralia kali, fistula na kuharibika kwa mimba na magonjwa ya moyo.

 “Madhara mengine yanayowakabili wanawake  ni kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua na kukosa msaada na jambo hilo linauwezakao mkubwa wa kusababisha vifo kwa mama na hata kwa mtoto pia.”alisema Norah.

Norah alieleza kuwa, kuna umuhimu mkubwa mwanaume kufika na mke wake kliniki ili waweze kupata elimu juu ya afya ya uzazi, lakini pia kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi ninavyosababisha ukimwi.

 “Tumekua tukitoa ushauri kwa kina mama wajawazito kila wanapokuja kliniki kupima, lakini pia tunashauri kufika na waume zao ili kujua upana na hatari ya matatizo wanayoweza kuwa nayo, pia kuwapa maelekezo ya kufanya pale mama atakapogundulika kuwa na tatizo,” alisema Norah.

Afisa Mtendaji Kata ya Jinjimili, Patrick Damson alieleza kuwa, wanawake walio wengi wanakumbana na madhara hayo, kutokana na kutohudhuria kliniki kwa wakati na hii huweza kusababishwa pia na uduni wa maisha ya wakazi wa vijiji hivyo.

Sababu nyingine ni pamoja na  kushindwa kulipia gharama za Usafili pindi wanapotakiwa kufika katika vituo vya kutolea huduma za Afya kutokana na umbali uliopo kutoka nyumbani hadi kituoni.

Mganga mkuu Wilaya ya Magu, Dkt. Maduhu  Nindwa anasema uelewa finyu wa umuhimu wa kinga na hadhari ya wiki kabla ya siku ya kujifungua imekuwa chanzo cha matukio mengi ya vifo visivyo vya lazima. Asilimia 25 ya wanawake hao huko vijijini hawajaeleimika kikamilifu kwa kutofika kliniki.

 “Mwanamke mjamzito anapaswa kuanza kuhudhuria ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto tumboni mwake akiwa na miezi mitatu yaani ahudhurie kliniki kwa miezi sita kabla ya siku ya kujifungua apimwe na kupewa dawa stahili,” anasema Dkt. Maduhu.

Kutokana na hali hiyo, Mganga mkuu huyo aliomba  serikali ijitahidi kupunguza changamoto zinazosababisha afya ya Watanzania wengi hasa waishio vijijini kulegalega kutokana na kutotekelezwa kikamilifu kwa sera ya afya inayoelekeza kuwepo zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata.

No comments:

Powered by Blogger.