Mbunge jimbo la Ilemela avutiwa na kasi ya wakazi wa Kiseke
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Judith Ferdinand, BMG
Mbunge wa
Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza Mhe.Angeline Mabula amewahimiza wakazi wa Kata
ya Kiseke jimboni humo kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha ujenzi wa
shule ya sekondari ya Kata hiyo.
Mhe.Mabula ambaye
pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametoa rai hiyo
alipofanya mkutano wa hadhara katika Kata hiyo na kubainisha kwamba urithi
pekee kwa mtoto hivi sasa ni elimu.
Alisema
ujenzi wa shule hiyo ukikamilika wanafunzi wataondokana na adha ya kutembelea
umbali mrefu na hivyo kuondokana na changamoto kadhaa ikiwemo vishawishi
hususani kwa watoto wa kike na hivyo kujiepusha na mimba za utotoni.
Mhe.Mabula
alisema wananchi wakishiriki kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa
kwa kunyanyua boma, serikali pamoja na ofisi yake itawaunga mkono kwa
kukamilisha majengo hayo ambapo alitumia mkutano huo kuendesha harambee fupi na
kufanikiwa kuchangisha shilingi 125,200, mifuko ya saluji 69 pamoja na tripu 12
za mawe.
Naye Mkurugenzi
Manispaa ya Ilemela, John Wanga aliwapongeza wananchi wa manispaa hiyo kwa
kujitoa kushirikiana na serikali katika miradi ya maendeleo na kuwahimiza
kuendelea na desturi hiyo kwa manufaa yao.
Katika
kuunga mkono juhudi za wananchi, Meneja wa benki ya NMB tawi la Rock City,
Jacqueline Timoth alisema benki hiyo inaunga mkono juhudi za maendeleo katika
jamii hivyo itasaidia ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari Kiseke.
Awali Afisa
Mtendaji wa Kata ya Kiseke, Hellen Mcharo alisema zinahitajika shilingi Milioni
102.58 ili kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo ambayo itakuwa na vyumba vinne
vya madarasa, ofisi vyumba vitatu na choo chenye matundu 12 ambapo matundu 10 yatakuwa
ya wanafunzi na mawili walimu.
No comments: