Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko afanya ziara mgodi wa Makaa ya Mawe mkoani Ruvuma
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kulia mbele) na Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma, Christina Mndeme (katikati) wakiendelea na ziara katika eneo la
mgodi wa Tancoal uliopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma jana tarehe 17 Julai, 2018.
Na Greyson Mwase, Mbinga
Naibu Waziri wa Madini,
Dotto Biteko jana tarehe 17 Julai, 2018 amefanya ziara katika mgodi wa
Makaa ya Mawe wa Tancoal uliopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Katika msafara wake aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Maafisa Madini
wa Songea, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga,
pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Mbinga.
Mara baada ya kufika katika mgodi huo na kupewa taarifa juu ya shughuli za uendeshaji wa mgodi huo,
Naibu Waziri Biteko aliagiza mgodi huo kuhakikisha unalipa kodi stahiki
ya madini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross
value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).
“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa
kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa
madini hayo na si hapa mgodini, na ninatoa mwezi mmoja mhakikishe mmerekebisha
kasoro zote na fedha ambazo hazikulipwa zilipwe. Ninatamani mimi niwe wa mwisho
kuliongelea suala hilo, migodi mingine yote imeshaanza kutekeleza sheria hii
sijui kwanini mmebaki ninyi,”alisema Biteko.
Alisema ni wakati sasa kwa wananchi wa Tanzania kunufaika na
rasilimali za madini kupitia kodi stahiki ambazo zinatumika katika kukuza sekta
nyingine ikiwa ni pamoja na huduma za
kijamii.
Alisisitiza kuwa, endapo hatua husika hazitachukuliwa, Serikali
kupitia Wizara ya Madini itaandikia mgodi hati ya makosa itakayopelekea
kunyang’anywa leseni ya uchimbaji na uuzaji wa madini.
Aliongeza kuwa ni jukumu la kampuni ya Tancoal kusafirisha madini
hadi eneo la wanunuzi kwa kuwa wana leseni za uchimbaji na uuzaji na si
wanunuzi wasio na leseni hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria za Madini.
Pamoja na kuitaka kampuni ya
Tancoal kufanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria alishauri kampuni
hiyo kufanya kazi kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na mbia wake ambaye ni
Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kupitia usimamizi wa uzalishaji, upimaji, usafirishaji na
uuzaji wa madini.
Aidha, Naibu Waziri
alisikitishwa na kitendo cha NDC kutokuwa na mwakilishi wake hapo mgodini
toka mwaka 2016 baada ya afisa aliyekuwepo kustaafu.
“ Ninajua NDC hampo Wizara ya Madini, lakini mpo Serikalini na
mimi ni Naibu Waziri wa Serikali hii ninawashauri mlete haraka mwakilishi
kwenye mgodi huu ili kuwepo na jicho la NDC kama mbia kwenye mgodi huu badala
ya kutegemea taarifa za mbia wenu tu ambaye ni Tancoal,”alisisitiza.
Wakati huo huo akizungumza katika mkutano wake na wachimbaji
wadogo wa madini, Naibu Waziri Biteko alisema kuwa mara baada ya taratibu kukamilika leseni za
biashara ya madini zinatarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa mwezi huu na
kuwataka kujiandaa na soko litakalotokana na wanunuzi wengi watakaojitokeza.
Katika hatua nyingine, Biteko aliwataka maafisa madini nchi nzima
kusikiliza kero za wachimbaji wadogo wa madini pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.
Aliwataka wachimbaji madini kuhakikisha wanafanyia leseni zao kazi
na zile ambazo zitaonekana hazifanyiwi kazi kwa muda mrefu zitafutwa na kupewa
wachimbaji wadogo.
Aidha alisisitiza wamiliki wa migodi ya madini nchi nzima kuajiri watanzania wenye uwezo
kama Sheria ya Madini inavyofafanua
badala ya kuajiri raia wa kigeni tu.
Aidha, Naibu Waziri Biteko mbali na kumpongeza Rais John Magufuli
kwenye usimamizi wa rasilimali za nchi, aliwataka wachimbaji wa madini kumuunga
mkono kupitia uzalendo kwenye usimamizi wa madini kwa manufaa ya Taifa.
“Tunataka madini haya baada ya miaka kadhaa yalete matunda kama
vile huduma za jamii hususan elimu, hospitali, barabara nzuri n.k” alisisitiza
Biteko.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme mbali na kumpongeza
Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa anayofanya katika usimamizi wa sekta ya
madini alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga kupima maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa
madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara kati ya wachimbaji hao na wakulima
au wafugaji.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiangalia moja ya
jiwe la makaa ya mawe. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akitoa maelekezo
kwa baadhi ya watumishi wa kampuni ya Tancoal.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na wachimbaji
wadogo wa madini (hawapo pichani) katika eneo Masuguru lililopo wilayani Mbinga
mkoani Ruvuma.
Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini katika eneo Masuguru
lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri
wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani).
No comments: