Naibu Waziri Biteko atatua mgogoro uchimbaji madini Tarime
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Naibu Waziri
wa Madini, Doto Biteko (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime,
Glorious Luoga (kushoto) mara alipowasili katika wilaya hiyo kwa ajili ya
kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali
za wachimbaji wa madini.
Na Greyson Mwase, Tarime
Naibu Waziri
wa Madini, Doto Biteko ametatua mgogoro kwenye machimbo ya madini ya dhahabu
ya Msege yaliyopo wilayani Tarime
mkoani Mara kwa kuitaka kampuni inayojishughulisha
na uchimbaji wa madini hayo ya Everson Limited kuhakikisha inasaini mikataba
kati yake na wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli za uchimbaji
madini na kushirikiana kwa karibu zaidi.
Naibu Waziri
Biteko ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea machimbo hayo jana Septemba 19, 2018 na
kusikiliza kero za wachimbai wadogo wa madini
ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Mara na Geita yenye lengo la kukagua shughuli za
uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini.
Katika hatua
nyingine, Biteko alimtaka mmiliki wa kampuni ya Everson Limited, Mwita Wambura
kuhakikisha anasimamia makubaliano aliyojiwekea kati ya wachimbaji wadogo wa
madini na kampuni yake huku akihakikisha sheria na kanuni za uchimbaji wa
madini zinafuatwa.
Alisema kuwa
mara baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili yaani kampuni na
wachimbaji hao alibaini kuwa kampuni husika ilikataa kusaini mikataba kati yake
na wachimbaji wadogo wa madini kinyume na makubaliano hali iliyopelekea mgogoro
kutokuisha.
“Haiwezekani
kama kampuni mnakaa katika vikao kwa kushirikisha viongozi wa serikali na
kukubaliana kuandaa mikataba ili kusaini halafu baadaye mnashindwa kutekeleza
makubaliano, kama Serikali tunataka kuhakikisha kila upande unanufaika, huku
Serikali ikipata mapato yanayostahili,” alisisitiza Biteko.
Aliendelea
kusema kuwa, Serikali ina haki ya kuchukua leseni ya kampuni yoyote pale inapoonekana makubaliano kati
yake na wachimbaji wadogo hayafuatwi hali inayosimamisha kukwama kwa shughuli
za uchimbaji madini na kukosa mapato yake.
Wakati huo
huo wananchi kutoka sehemu mbalimbali katika Wilaya ya Tarime walimpongeza
Naibu Waziri Biteko kwa kuhakikisha kuwa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu
pasipo kupatikana suluhu unatatuliwa ndani ya kipindi kifupi na kusisitiza kuwa
wataendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Madini kwa kuhakikisha wanafuata
sheria na kanuni za madini huku wakilipa
kodi zote serikalini.
Akizungumza
kwa niaba ya wachimbaji wa madini, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini
Mkoa wa Mara, Stephan Msseti alimpongeza
Biteko kwa kuhakikisha amefika kwenye machimbo hayo na kutatua mgogoro na
kufafanua kuwa sasa wachimbaji wadogo wataanza kuchimba katika mazingira ya
amani na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Msseti
alimtaka mmiliki wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Everson
Limited, Mwita Wambura kuhakikisha anaheshimu mamlaka za serikali kwa
kuhakikisha anatekeleza makubaliano yote wanayojiwekea.
Awali
akizungumzia mgogoro huo, mmiliki wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu
ya Everson Limited, Mwita Wambura alisema kuwa mara baada ya kufanya utafiti na
kuanza uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo hilo, wananchi walianza
kuvamia eneo hilo hali iliyopelekea
mgororo.
Alisema kuwa
aliwaruhusu wachimbaji wadogo kuchimba madini katika mashimo matano lakini
wachimbaji hao wamekuwa wakidhuru wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kuwapiga kwa
kuwa si wakazi wa kijiji husika kauli ambayo ilipingwa na Diwani wa Kata wa
Nyarukoba kupitia CHADEMA, Matiko Marwa.
Marwa mbali
na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara
ya Madini alimtaka mwekezaji huyo kutii makubaliano kwa kusaini mikataba ili
kumaliza mgogoro.
Kabla ya
kufanya ziara katika machimbo hayo, Naibu Waziri Biteko alikutana na Mkuu wa
Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na kuelezwa changamoto mbalimbali
zinazoikabili Wilaya hiyo hususan kwenye
uchimbaji wa madini.
Luoga
alieleza changamoto hizo kuwa ni pamoja na
ukusanyaji wa maduhuli kuwa mdogo kutokana na wachimbaji wadogo wengi
kuchimba madini pasipo kutambulika, baadhi ya wachimbaji wadogo kuwepo
kwenye leseni zenye uwekezaji,
utoroshwaji wa mawe yenye dhahabu na migogoro katika baadhi ya maeneo yenye
shughuli za uchimbaji madini.
Naibu Waziri
wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika
Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime.
Naibu Waziri
wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na
ziara katika machimbo ya dhahabu ya Msege
yaliyopo wilayani Tarime mkoani Mara
Naibu Waziri
wa Madini, Doto Biteko akiangalia sehemu ya nyaraka mbalimbali za uchimbaji
madini katika machimbo ya dhahabu ya
Msege yaliyopo wilayani Tarime
mkoani Mara.
Mmoja
wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika machimbo ya dhahabu ya
Msege yaliyopo wilayani Tarime mkoani
Mara akiwasilisha kero yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko
Sehemu
ya wananchi wa kijiji cha Msege kilichopo wilayani Tarime mkoani Mara
wakisikiliza ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto
Biteko
Naibu Waziri
wa Madini, Doto Biteko akitoa maelekezo kwa mmiliki wa kampuni inayojishughulisha
na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Kisege Wilayani Tarime Mkoani
Mara ya Everson Limited, Mwita Wambura (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza
katika mkutano wa hadhara
No comments: