Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula waonya kuhusu ubora wa mahindi
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Vumilia
Zikankuba
Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma
Ikiwa msimu wa kununua mazao umeanza,
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA),
Vumilia Zikankuba amewataka wakulima
kuhakikisha wanazingatia ubora wa mahindi.
Aidha, amesema nchi inachakula cha
kutosha na kusisitiza kuwa katika msimu wa kwanza wa ununuzi wa mahindi bei ya
NFRA ni wastani wa Sh 380 hadi Sh 400 kwa kilo.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake Mjini Dodoma, Zikankuba alisema NFRA haitaweza kununua mahindi
mabovu na kusisitiza wakulima kuwa na mahindi yenye ubora ambayo yatawasaidia
kupata masoko ya nje pia.
"Haiwezekani NFRA itumia fedha za
Serikali kununua mahindi yasiyokidhi viwango vya ubora na machafu kutoka kwa
wakulima. Hivyo wakulima wanapaswa kuzalisha mahindi kwa kuzingatia viwango vya
ubora vinavyokidhi vigezo vya soko.
Aliongeza: “Lazima chakula
tunachonunua kizingatie ubora. Tunataka tubadilishe taswira ya NFRA kwa sababu
awali kulikuwa na tatizo la chakula kuharibika kwa kipindi kifupi.”
Zikankuba alisema ili kuhakikisha
mahindi ya wakulima yanaweza kukidhi viwango vinavyotakiwa NFRA tayari
imekwishatoa elimu kwa wakulima kupitia vikundi na kwenye vyombo vya habari.
Alibainisha kuwa baada ya elimu hiyo
wakala umefanikiwa ambapo wakulima kutoka maeneo ya Makambako, Sumbawanga na
Mpanda wameanza kuzalisha na kuuza mahindi yenye ubora kwa NFRA.
“Changamoto iliyopo ni kwa baadhi ya
wakulima wachache ambao bado wamekuwa wagumu kubadilika na wale ambao wanaamini
wakitumia nafasi zao wanaweza kuuza mahindi yasiyo na ubora,"
Alisema kwa mkulima kuwa na mahindi
yenye ubora unatoakiwa utasaidia katika kupata soko la NFRA, pia katika taasisi
zingine zinazonunua nafaka hiyo za ndani na nje ya nchi.
"Dhima ya serikali ni kwenda
uchumi wa kati kupitia uchumi wa viwanda, kwa mahindi pekee hayatumiki kwa
chakula pekee, bali kutengeneza bidhaa mbalimbali. Hivyo hatuwezi kufikia
Tanzania ya viwanda endapo wakulima watazalisha malighafi zisizokuwa na ubora,”
alieleza.
Viwango vinavyopaswa kuzingatiwa na
wakulima wa mahindi ni kwamba unyevunyevu usizidi asilimia 13.5, takataka
asilimia 0.5 na punje zilizovunjika zisizidi kwa asilimia 2.
Viwango vingine ni punje zilizoliwa na
wadudu na zilizosinyaa zisizidi asilimia moja, punje mbovu asilimia mbili na
punje za rangi tofauti zisizidi asilimia 0.5.
Zikankuba alitoa msisitizo kwa
wakulima kutunza chakula badala ya kukiuza chote.
“Msimamo wa Rais (John Maguful) wa
kutotoa chakula cha msaada upo sahihi kwa sababu kuna maeneo walikwishazoea
kupelekewa chakula cha msaada. Msimamo huo umelenga kuwahamasisha wananchi
kutunza chakula, haya malalamiko ya hatuna chakula yanachangiwa na uzembe wa
wananchi wa kuuza chakula chote,” Vumilia, alibainisha.
Alisema jukumu la wakala ni kutunza
chakula kwa ajili ya dharura kama kumetokea majanga kama mafuriko, njaa,
tetemeko na majanga mengine ambayo
wanachi watahitaji msaada wa chakula.
Kuhusu bei ya mahindi ambayo NFRA
imeanza kununua mahindi kwa wakulima Zikankuba alisema ni wastani wa Sh 380 kwa
kilo hadi Sh 400 kwa kilo kulingana na eneo na eneo, na ni bei inayoendana na
mwenendo wa bei ya soko.
“Mfano bei ya soko ya mahindi mkoani Ruvuma ni
Sh 250 kwa kilo, lakini sisi kama NFRA tunanunua kwa bei ya juu ya kuanzia Sh
350 hadi 380 kwa kilo," alisema.
Aliongeza: “Mkoani Dodoma NFRA
inanunua Sh 420 kwa kilo, Makambako Sh
400, Shinyanga Sh 500, Katavi na Ruvuma Sh 350 hadi 380. Bei hiyo bado ni ya
juu ukilinganisha na bei ya soko iliyopo,” alifafanua.
Aidha, Zikankuba alisema ziada ya
mazao yote yaliyozalishwa na wakulima msimu huu imefikia tani milioni 2 huku
ziada ya mahindi pekee ni tani 970,000.
Zikankuba alisema NFRA imetengewa Sh
bilioni 15 kwa ajili ya kununua tani 28,000 kwa awamu ya kwanza ikiwa ni
asilimia 2 ya ziada ya mahindi iliyopo.
Zikankuba alisisitiza kuwa NFRA
inazingatia ubora wakati wa kununua kwa kuwa ni haki na muhitaji kupatiwa
chakula bora na Salama kwa afya wakati
wa dharula hivyo mahindi ambayo hayana ubora yakituzwa kwa muda mrefu ghalani
yanakuwa na nafasi kubwa kupata vimelea vya fangasi ambao husababisha uwepo wa
sumu kuvu katika nafaka hiyo.
Alisema kuwa Sumu kuvu ni hatari sana
kwa afya ya mlaji. Tatizo hili kwa kiasi kikubwa sana, linaweza kuepukika kwa
mkulima kufuata mbinu bora za kilimo, mbinu bora za utayarishaji nafaka na
mbinu bora za kuhifadhi nafaka baada ya kuvuna. Lengo la NFRA ni kutoa chakula
chenye ubora na salama wakati wa dharura.
No comments: