Serikali kupambana na mimea vamizi Ngorongoro
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Pichani ni
mmea vamizi ambao unaathiri sana malisho ya wanyama katika bonde la Ngorongoro
kreta. Serikali inachuka hatua za haraka kudhibiti mmea huo unaosambaa kwa
kasi.
Na Mwandidhi Maalum
Serikali
imeazimia kurudisha ikolojia ya hifadhi ya Ngorongoro katika mazingira yake ya
asili na kusisitiza kuwa shughuli zote za kuharibu na kuchafua ikolojia hiyo
vitadhibitiwa kwa nguvu na uwezo wote.
Akizungumza
na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba amesema kuwa lengo la
ziara yake ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mamlaka hiyo
mwezi Machi 2017.
Katika ziara
yake mapema mwaka jana pamoja na mambo mengine Waziri Makamba aliagiza Mamlaka
hiyo kuchukua hatua za haraka na kuwaelekeza wamiliki wa hoteli na loji hususan
zilizoko katika kingo za kreta katika bonde la Ngorongoro kutafuta vyanzo
mbadala vya maji na kuondokana na kutegemea chanzo cha chemichemi za Lerai.
Aidha,
Waziri Makamba aliagiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kudhibiti mimea
inayohatarisha uoto wa asili katika Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuunda jopo la
wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Tecknolojia, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira, Hifadhi za Taifa za Tanzania, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Mamlaka
ya Ngorongoro ili kufanya utafiti wa kina na wakisayansi wa kubaini mbinu mpya
ya kupambana na mimea hiyo vamizi inayotawala mimea inayotumiwa na wanyama kama
malisho.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro Dkt. Maurus
Msuha amesema kuwa Mamlaka ya Ngorongoro iliwaandikia barua wamiliki wote wa
hoteli na loji na kufanya tafiti kupitia
kwa wataalamu elekezi wawili tofauti ambao kwa pamoja walishauri kuandaliwa kwa
mkakati wa usimamizi na matumizi ya maji ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro
utakaokuwa suluhisho la matatizo la maji bila kuathiri mifumo ya ikolojia
katika Hifadhi.
Aidha,
katika kukabiliana na changamoto ya mimea vamizi ndani ya hifadhi, Bw. Msuha
amesema kuwa Mamlaka imeanda ramani ya kuainisha aina, kiasi na maeneo ilipo
mimea vamizi ndani ya hifadhi ili kuweza kuweka mikakati na mbinu sahihi za
kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na kuendelea na kazi ya kutumia njia rafiki ya
kimazingira ya kungo’a, kufyeka na kuchoma njia iliyoonyesha mafanikio makubwa
hususan katika kudhibiti mmea tishio (Darura stramonium) ndani ya kreta na
maeneo mengine.
Bw. Msuha
amefafanua kuwa Ofisi yake inashirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Sayansi na
Teknoljia ya Nelson Mandela ya Mkoani Arusha na wameanziasha utafiti utakaodumu
kwa kipindi cha miaka miwili, utafiti wa kuua magugu katika hifadhi kwa kutumia
mifumo ya ki-biolojia. Matokeo ya awali yanaonyesha mafanikio kwa asilimia 70
katika kupambana na mimea vamizi.
Mara baada
ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Makamba amesema kuwa suala la mimea vamizi ni
janga la kitaifa ambalo kwa sasa linawekewa mikakati ya kitaifa ili kuweza
kukabiliana nalo. “Mimea hii vamizi imetapakaa maeneo mengi nchi hivyo jitihada
za pamoja zinahitajika, Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tumeitisha Mkutano Mkubwa
Arusha tarehe 04/09/2018 utaojumuisha wataalamu na wadau kutoka taasisi
mbalimbali ili kwa pamoja tuzungumze chanzo cha tatizo hili, ukubwa wake,
madhara na hatua za kuchukua” Makamba alisisitiza.
Pia, Waziri
Makamba ametoa muda wa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Ngorongoro kuanza kutekeleza
kwa vitendo Mpango wa usimamizi na matumizi ya maji ndani ya Mamlaka na kutoa
rai kwa wamiliki wa Hoteli na loji hususan zilizoko katika kingo za kreta
katika bonde la Ngorongoro kuanza kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya
kutibu maji taka ili yaweze kutumika tena na kuwataka kufahamu kwa matumizi ya
maji kutoka ndani ya kreta hitimisho lake linakaribia.
Waziri
Makamba yuko Mkoani Arusha kupitia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa mwaka
jana pamoja na kuzungumza na wadau waliowekeza katika hoteli na kambi za
uwindaji.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akipata
maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Dkt. Linus Munishi mtafiti kutoka Taasisi ya
Nelson Mandela. Taasisi hiyo imetenga eneo maalumu la majaribio ya kuua mimea
vamizi bila kuathiri mazingira, utafiti unao onekana kufanikiwa.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akiwa katika
kikao na wadau na wamiliki wa hoteli zilizopo katika kingo za kreta katika
bonde la Ngorongoro. Pamoja na mambo mengine Waziri Makamba amewata kuwekeza
katika teknolojia ya kisasa ya kutibu maji taka ili yaweze kutumika tena na
kuwataka kufahamu kwa matumizi ya maji kutoka ndani ya kreta hitimisho lake
linakaribia, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro.
No comments: