Nyongo aagiza Afisa Madini, Watendaji kusimamia ufungaji na ufunguaji wa madini
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiangalia sampuli
ya makinikia ya dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo
katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akisalimiana na
sehemu ya wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika
eneo la Singililwa lililopo Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati)
akiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo
katika eneo la Singililwa Wilayani
Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa nne kulia)
akikagua shughuli za uchenjuaji wa dhahabu zinazofanywa na wachimbaji wadogo
katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi.
Na Greysona Mwase
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Afisa Usalama wa Wilaya, na Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanakuwepo wakati wa ufungaji na ufunguaji wa lakiri (seal) kwenye madini ya dhahabu ili kudhibiti utoroshwaji wa madini kwenye migodi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Afisa Usalama wa Wilaya, na Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanakuwepo wakati wa ufungaji na ufunguaji wa lakiri (seal) kwenye madini ya dhahabu ili kudhibiti utoroshwaji wa madini kwenye migodi.
Aliyasema
hayo juzi baada ya kumaliza ziara yake katika Mgodi Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la
Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi
ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika
mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli
za uchimbaji wa madini, kusikiliza na
kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara
yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Salehe Mhando, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini
Mkoa wa Katavi (KATAREMA), William Mbongo, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Wataalam wa Madini, Vyombo vya Ulinzi na
Usalama pamoja na waandishi wa habari.
Alisema
kuwa, ni kosa kubwa la kisheria kwa Afisa Madini Mkazi kufunga au kufungua
lakiri (seal) pasipo kushirikisha Mkuu
wa Wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
kusisitiza kuwa iwapo itagundulika Serikali haitasita kuchukua hatua kali za
kisheria.
Akielezea
mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya
Madini Nchini, Nyongo alisema kuwa ni pamoja na uboreshaji wa Sheria ya Madini
iliyolenga kuondoa mianya ya utoroshwaji wa madini nje ya nchi kwa kuzuia
usafirishwaji wa madini ghafi nje ya nchi.
Alisisitiza
kuwa, Serikali inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika
ujenzi wa mitambo ya kuchenjulia madini ndani ya nchi ili kuyaongezea thamani kabla ya kuuzwa nje ya
nchi na kuongeza mapato.
Wakati
huohuo akizungumza katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi yanayomilikiwa na William Mbogo, Naibu Waziri
Nyongo alimtaka mmiliki wa leseni kuhakikisha anaandaa mikataba na kusaini
pamoja na wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika
eneo hilo.
Alisema
kuwa, Serikali kupitia Wizara yake haipo tayari kushuhudia migogoro kati ya
wawekezaji na wachimbaji wadogo wa madini pasipo suluhu inayotokana na
ukiukwaji wa Sheria za Madini na kanuni zake.
Katika hatua
nyingine, Nyongo alimtaka mwekezaji huyo kutafuta mwekezaji mkubwa kwa ajili ya
usimamizi wa shughuli za uchimbaji madini katika eneo husika iwapo anakosa
uwezo wa kuendeleza kama leseni ya madini inavyomtaka.
Aidha,
alimwelekeza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard
Luyoka kuhakikisha anatafuta maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini,
ili waweze kuchimba katika mazingira mazuri huku wakifuata sheria na kanuni za
madini.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha
wanalipa mrahaba na kodi mbalimbali Serikalini ili mapato yaweze kutumika
kwenye uboreshaji wa sekta nyingine kama
vile afya, elimu, maji na miundombinu.
Awali mbali
na pongezi, wakiwasilisha kero mbalimbali wachimbaji wadogo wa madini
wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba
yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi yanayomilikiwa na William Mbogo walieleza
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji midogo, vifaa duni pamoja
maeneo rasmi kwa ajili ya uchimbaji madini.
No comments: