LIVE STREAM ADS

Header Ads

Halmashauri ya Mji Geita yaja na mkakati wa kupambana na "madada poa"

Wasiliana na BMG Blog/ BMG Online TV kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma ya Habari na Matangazo.

Na Joel Maduka, Geita
Baraza la madiwani wa halmashauri ya Mji wa Geita limeeleza kuweka mikakati ya kuhakikisha linapambana vikali na akina dada ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara haramu ya ngono kwa kubomoa nyumba ambazo wamekuwa wakiishi na kufanya biashara hiyo.

Hoja ya uwepo wa biashara hiyo haramu ilibuliwa na madiwani wakati wa kikao ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo ambapo katika kipindi cha maswali na majibu madiwani hao wakataka kujua nini mikakati ya halmashauri kuhakikisha inadhibiti biashara hiyo ambayo imeendelea kuota mizizi kila wakati kwenye maeneo ambayo yamekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu.

"Pamoja na kwamba tupo kwenye mapambano ya kuwadhibiti madada poa lakini kwenye halmashauri yetu tumeshuhudia baadhi ya watumishi kuvaa mavazi ambayo hayaendani na maadili yetu ya kitanzania, mkakati wa halmashauri ukoje katika kuhakikisha kwamba wanadhibiti suala hili la mavazi ambayo yamekuwa sio mazuri hata kwa kutazama kwa macho?". Aliuliza diwani Elias Ngolle.

Kufuatia swali hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mhandisi Modest Aporinaly alisema tayari amekaa na kamati ya ulinzi na usalama katika kuhakikisha wanadhibiti maeneo ambayo yamekuwa yakifanya biashara hiyo haramu.

"Naomba ni wahakikishie tu waheshimiwa tayari tunao mchakato wa kubomoa vibanda ambavyo vimeonekana kuendelea kuwahifadhi madada hawa, na kuhusu mavazi kwa watumishi tayari tumeweka sheria na imeshaanza kutumika na sio kwa watumishi tu hata mwananchi wa kawaida anapokuja hajavaa mavazi ambayo ni mazuri walinzi wamekuwa wakiwarudishia getini". Alisema Aporinaly.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita, Leornad Bugomola alisema kuondolewa kwa "madada poa"wanaofanya biashara haramu ya ngono kutasaidia kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika jamii.

Katika taarifa aliyotolewa hivi karibuni na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kipindi cha kuanzia Mwenzi Julai Hadi Septembar mwaka huu, idadi ya waliobainika kuwa na maambukizi ya VVU ni 383 ambapo wanawake ni 218 na wanaume 165.

No comments:

Powered by Blogger.