LIVE STREAM ADS

Header Ads

Raia wa China anaswa na TAKUKURU akijaribu kutoa rushwa kwa Mkuu wa Mkoa Geita

Wasiliana na BMG Blog/ BMG Online TV kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma ya Habari na Matangazo.

Na Joel Maduka, Geita
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Geita imemfikisha Mahakamani raia mmoja wa China, Cheng Li ambaye ni mfanyabiashara wa madini kwa tuhuma za kushawishi na kujaribu kutoa rushwa kwa mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel kinyume na kifungu cha 15 (1) (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kwamba mtuhumiwa alifikishwa mahakamani Disemba 06, 2018 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita Mhe. Jovith Kato ambapo alisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Dennis Lekayo.

Mwendesha Mashitaka aliieleza Mahakama kwamba kati ya Oktoba 2018 na Novemba 10, 2018 mshitakiwa alimshawishi Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel kwa njia ya ujumbe wa simu kumpatia kiasi cha Shilingi Milioni Moja kila mwezi na kwa kuonesha kuwa alidhamiria kutoa rushwa hiyo, mshitakiwa alimtumia ujumbe mwingine Mhandisi Gabriel akimshawishi kumpelekea kiasi cha shilingi Milioni moja na paketi ya majani ya chai kutoka nchini China.

Baada ya kupokea ujumbe huo, Mhandisi Gabriel alitoa taarifa ofisi ya TAKUKURU Mkoa Geita, ambapo mtego uliandaliwa na kufanikiwa kumkamata mshitakiwa akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa tayari akiwa amejiandaa kutoa rushwa hiyo ya shilingi Milioni moja na pakiti ya majani ya Chai kama alivyokuwa ameahidi kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.

Mshitakiwa alisomewa mashitaka yanayomkabiri na kuyakana yote ambapo Hakimu alitaja masharti ya dhamana kuwa ni wadhamini wawili wa kuaminika watakao saini fedha ya ahadi kiasi cha shilingi Milioni mbili kila mmoja na mshitakiwa kuwasilisha Hati ya Kusafiria Mahakamani ambapo mshitakiwa alitimiza mashariti ya dhamana na kesi kuahirishwa hadi Disemba 20, 2018.

No comments:

Powered by Blogger.