Waziri Biteko asisitiza mgodi wa North Mara kuwalipa wananchi fidia zao
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa madini, Doto Biteko (kushoto) akihoji jambo kwa viongozi
wa mgodi wa North Mara uliopo Wilaya ya Tarime mkoani Mara, waliofika ofisini kwake Jijini Dodoma kumpa mrejesho wa
kinachoendelea katika utekelezaji wa majukumu yao na maagizo ya Serikali ikiwemo ulipaji fidia za wakazi wanaozunguka mgodi huo.
Viongozi wa mgodi wa North Mara nchini wakiwa katika kikao
na Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kilichofanyika katika ofisi
za wizara jijini Dodoma.
Msaidizi wa Waziri Kungulu Masakala (wa Kwanza Kushoto),
Wawakilishi kutoka Tume ya Madini, na
Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Sera na Mipango Glads Qambaita wakiwa katika
kikao baina ya Wizara ya Madini chini ya Waziri, Doto Biteko (hayupo
pichani) na uongozi wa mgodi wa North
Mara.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (kulia), akihoji uhalali
wa Maelekezo ya Seikali kupingwa na viongozi wa Mgodi wanaoishi nnje ya
Tanzania (Uingereza na Afrika Kusini) na wasioshiriki katika vikao vya mamuzi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko, akiwasomea viongozi wa north
Mara baadhi ya taarifa alizonazo juu ya
masuala ya tathmini za fidia ya ardhi zilizofanywa na matokeo yake pamoja na
kile wanachopaswa kuwa wamekitekeleza mpaka siku ya kikao hicho tarehe 17
Januari, 2019.
Mkurugenzi wa masuala ya kijamii katika mgodi wa North Mara,
Richard Ojendo akieleza jambo mbele ya Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo
pichani) katika kikao kilichofanyika katika ofisi za wizara jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akipiga simu kwa Mthamini Mkuu
wa Serikali (jina halikupatikana mapema) kuhoji juu ya kile viongozi wa North
Mara wanadai kuwa changamoto katika kutekeleza suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Katibu Mkuu wa madini, Prof. Simon Msanjila (kushoto)
akieleza jambo katika kikao baina ya viongozi wa juu wa wizara na viongozi wa
mgodi wa North Mara kilichofanyika tarehe 17 Januari, 2019 ofisini kwa Waziri
wa Madini, Doto Biteko (kulia) jijini Dodoma.
Na Nuru Mwasampeta, Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko pamoja Katibu Mkuu Wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila wamekutana na uongozi wa mgodi wa dhahabu wa North Mara na kuutaka kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Akizungumza jana kwenye kikao hicho kilichoketi katika ofisi ya waziri Jijini Dodoma, Biteko aliwaeleza wajumbe hao kuwa walipaswa kuwa wamechukua hatua kadhaa kuonesha kua wanatii maagizo ya Serikali lakini kutokana na wao kuhisi serikali haina cha kufanya wakaamua kutulia kwa miezi mine ambapo wamefika ofisini kueleza masuala ambayo hayajafanyiwa kazi.
“Hatuwezi kuwa tunakaa, tunafikia maamuzi ninyi mnayapinga, ni nani yupo juu ya Serikali” Waziri Biteko alihoji. “Mnajua suala la ardhi ni kubwa sana, mnajua ni maelekezo ya Rais, sasa Rais ameagiza halafu hakitokei kitu! Mimi sielewi kabisa. Afadhali watu wangeanza kulipwa unaweza sema sasa hatua za malipo zinafanyika”alikazia.
Sambamba na hilo Biteko aliwaeleza wajumbe hao kuwa uongozi wa mgodi huo hawamfuati mtu mahususi katika kutatua suala hilo na kubainisha kuwa mgogoro huo hautatatuliwa na wizara ya Madini isipokuwa ni watu wenye mamlaka na masuala ya ardhi.
Akizungumzia chanzo cha mgogoro kuchukua muda mrefu Biteko alieleza kuwa tatizo la kuongezeka gharama za malipo kumetokana na mgodi kuchelewesha malipo ya tathimini ya awali ambayo ilikuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.6, hii imepelekea kufanyika kwa tathimini ya pili iliyopelekea kufikia kiasi kikubwa cha bilioni 12 ukilinganisha na kile cha awali.
Hii ni kutokana kwamba, mara baada ya tathmini kufanywa kwa ajili ya malipo ya fidia, malipo yanapaswa kufanyika si zaidi ya miezi sita na baada tu ya tathmini kufanyika; aidha, mgodi ulipaswa kutoa tangazo ili kusimamisha uendelezaji wa maeneo kwani maeneo yakiendelezwa na tathmini kutolipwa kwa wakati kiasi kilichothaminishwa awali kinakuwa si dhahiri tena maana uwekezaji katika eneo husika unaongezeka.
Akifafanua hilo mara baada ya kuzungumza na mthaminishaji Mkuu wa Serikali kwa njia ya simu, Biteko alisema ameelezwa kwamba tathmini inayofuatwa ni ile iliyofanyika awamu ya pili maana hiyo ndiyo ya sasa na kukazia kuwa hawawezi kufuata ya awali kutokana na kwamba muda wa kuwalipa fidia hizo ulipaswa kutozidi miezi sita tangu tathmini kufanyika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Madini Prof Simon Msanjila alisema haiwezekani aje mtu asiyekuwa na maamuzi, Waziri atoe maamuzi halafu mtu aliyeko Uingereza ayapinge huu ni udhalilishaji, maamuzi ya mwisho yakishafanyinywa na Serikali hakuna serikali nyingine au kampuni iyapinge! Maamuzi yanayotolewa Tanzania hayawezi kwenda kujadiliwa London sio Sheria hiyo, ndio maana kampuni lazima iwe imesajiliwa Brella, kwa hiyo hakuna mambo ya kusema mshauri yupo London, South Africa. Alisisitiza
Msanjila aliwakumbusha kuwa makubaliano waliyoafikiana katika vikao vya nyuma kuwa endapo kiongozi yeyote wa North Mara anafahamu kuwa hana mamlaka ya kufanya maamuzi asihudhurie katika vikao vinavyolenga kupitisha maamuzi yazingatiwe.
Alipojaribu kujibu hoja hizo Bi Jane Reuben Lekashingo ambaye ni mmoja wa viongozi kutoka mgodi wa North Mara alisema kuwa kiongozi mkuu wa masuala ya kisheria katika mgodi huo yupo nchini Uingereza na kwamba endapo kunakuwa na suala lolote la kisheria ni sharti ashirikishwe ili kufanya maamuzi ya pamoja. Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila alihoji endapo north Mara ipo juu ya Serikali?
Prof. Msanjila aliendelea kwa kusema, Huyu ni waziri, anamwakilisha Rais, hamuwezi kwenda kuomba ushauri London kwa maagizo yaliyotolewa na waziri, hiyo si sheria, alikazia.
“Don’t talk about London or South Africa tunapoongelea masuala ya Tanzania tunaongea kwa sheria za Tanzania we have nothing to do with London hiyo ni yao” alisisitiza.
Baada ya mahojiano makali na yaliyochukua muda mrefu baadaye viongozi wa mgodi wa North Mara walielewa na kukiri kwamba baadhi ya wananchi waliofanyiwa tathmini ya malipo yako sahihi na kuahidi kufanya malipo, na kuahidi kwamba baada ya kufika katika vituo vyao vya kazi watakwenda kuendelea na taratibu za malipo ili kuonesha uungwana kwamba wamechukua hatua na kuonesha utii kwa mamlaka ya Serikali kwa kutii makubaliano yaliyoafikiwa na viongozi wakuu wa nchi.
Pamoja na kukiri kuwa wamejifunza kitu kutokana na kikao hicho viongozi hao walisema wataendelea kujifunza kwani wameona kuchelewa kwao katika kulipa fidia hizo kumeipelekea kampuni kutakiwa kutumia kiasi kikubwa cha pesa katika kulipa wananchi kutokana na shughuli za kimaendeleo walizoendeleza kuwekeza katika maeneo yao.
Aidha kutokana na uhalisia kisheria kuwa; tathmini ya ardhi ni hai kwa kipindi cha miezi sita na ikizidi hapo inafanyika tathmini nyingine lakini pia wamejifunza juu ya taratibu na sheria za kusitisha shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa kutangaza kusimamisha shughuli za maendeleo katika maeneo yaliyofanyiwa tathmini kwa kipindi cha miezi sita na pia kulipa fidia kwa wakati ili wananchi wakajiendeleze katika maeneo mengine watakayohamia.
No comments: