LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wachimbaji wadogo wa Madini Suguta mkoani Dodoma wapata leseni

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia) akimkabidhi leseni ya madini Mwenyekiti wa kikundi cha wachimbaji wadogo wa madini ya Sunstone katika machimbo ya Suguta yaliyopo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi Tu”, Elisha Cheti (kushoto).
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia), Mwenyekiti wa kikundi cha wachimbaji wadogo wa madini ya Sunstone katika machimbo ya Suguta wilayani Kongwa cha “Hapa Kazi Tu”, Elisha Cheti (katikati) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya makabidhiano hayo.

Na Greyson Mwase, Dodoma
Kikundi cha wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika machimbo ya Suguta yaliyopo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi Tu” kimepongeza Tume ya Madini kwa kutatua mgogoro uliokuwepo kwa muda mrefu pamoja na kuwapatia leseni.

Pongezi hizo zimetolewa leo katika makabidhiano ya leseni ya uchimbaji wa madini hayo katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma zilizopo jijini Dodoma.

Kutatuliwa kwa mgogoro kati ya kikundi hicho na wananchi wa kijiji cha Suguta ni matokeo ya ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliyoifanya mapema Septemba 05, 2018 katika machimbo hayo na kukuta kikundi hicho kikiendesha shughuli za uchimbaji wa madini pasipo kusajiliwa na kutokuwa na leseni ya uchimbaji wa madini.

Mara baada ya kufanya ziara katika eneo husika Profesa Kikula alielekeza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius John Ndejembi kuhakikisha kikundi cha wachimbaji hao kinasajiliwa na kupatiwa leseni ndani ya muda mfupi.

Aidha, Profesa Kikula alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto kuhakikisha mgogoro uliokuwepo kati ya kikundi hicho na wananchi wa kijiji cha Suguta unamalizika.

Akitoa shukrani hizo kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa kikundi cha “Hapa Kazi Tu” Elisha Cheti alisema kuwa ziara ya Profesa Kikula ilipelekea kuongezeka kwa kasi ya usajili wa kikundi na hatimaye wakafanikiwa kuomba leseni ya kuchimba madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma.

Alisema mara baada ya kupata leseni pamoja na barua ya utambulisho wanatarajia kuanza shughuli za uchimbaji madini na kulipa kodi na tozo mbalimbali Serikalini.

Naye Mwenyekiti wa DOREMA, Kulwa Mkalimoto mbali na kuipongeza na kuishukuru Tume ya Madini kwa utoaji wa leseni amekitaka kikundi kilichopewa leseni kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa kufuata sheria na kanuni za madini huku kikihakikisha hakuna uharibifu wowote wa mazingira.

Naye Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano akizungumza wakati wa makabidhiano hayo alifafanua kuwa, maombi ya leseni ya uchimbaji wa madini ya kikundi husika yalipitishwa kupitia kikao cha Kamati ya Ufundi ya Tume kilichokaa tarehe 22 Novemba, 2018.

Mwano alitoa wito kwa wachimbaji wadogo wasio rasmi kuunda vikundi, kusajili na kuomba leseni na kusisitiza kuwa ofisi yake itahakikisha leseni za madini zinatolewa kwa kasi ili waweze kuchimba pasipo kusumbuliwa huku wakilipa kodi na tozo mbalimbali Serikalini.

“ Sisi kama Tume, tunaamini wachimbaji wadogo wana mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa sekta ya madini; tunaunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli za kuhakikisha watanzania wote wananufaika na rasilimali za madini,” alisisitiza Mwano.

No comments:

Powered by Blogger.