LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kampuni ya Neelkanth yatakiwa kutumia malighafi za ndani kutengenezea chumvi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Mmoja wa Watendaji kutoka katika kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa chumvi ya Neelkanth Salt Limited iliyopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Mahendra Prasad (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo kwa Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki (kushoto) alipofanya ziara katika kampuni hiyo hii leo Februari 22, 2019 lengo likiwa ni kufanya ukaguzi pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Na Greyson Mwase, Pwani
Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki ameitaka kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa chumvi ya Neelkanth Salt Limited iliyopo Wilayani Mkuranga mkoani Pwani kuachana na uagizaji wa malighafi zinazotumika katika kuzalisha chumvi kutoka nje ya nchi na badala yake ijikite kwenye matumizi ya malighafi zilizopo nchini na kusisitiza kuwa kufanya hivyo kunazorotesha soko la ndani.

Dkt. Macheyeki alitoa agizo hilo mapema leo tarehe 22 Februari, 2019 kwenye ziara yake katika kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula katika mkoa wa Pwani yenye lengo la kutembelea wachimbaji wa madini pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Aliyasema hayo mara baada ya kuelezwa kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiagiza malighafi ya chumvi kwa asilimia kati ya 60 na 70 kutoka katika nchi za Namibia, India na Afrika ya Kusini.

Alisema kuwa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 inawataka wachimbaji wa madini nchini kutumia bidhaa za ndani ya nchi badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi na kuitaka kampuni hiyo kuendelea kujipanga zaidi katika kuhakikisha baadaye inaondokana na matumizi ya malighafi za kutoka nje ya nchi.

Aliendelea kusema kuwa, katika kujiandaa na matumizi ya malighafi ya chumvi kutoka ndani ya nchi, kampuni inatakiwa kutoa elimu kwa wazalishaji wa chumvi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Kilwa ili waweze kununua chumvi iliyo bora na kuondokana na matumizi ya malighafi ya chumvi kutoka nje ya nchi na kuinua uchumi wa wazalishaji hao wa chumvi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Macheyeki aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inawasilisha mpango wa manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho (local content plan) pamoja na kiapo cha uadilifu Machi 15 mwaka huu kwenye Ofisi za Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini zilizopo jijini Dodoma.

Aidha, Dkt. Macheyeki aliitaka kampuni hiyo kuwasilisha mpango wa kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi wake ili baadaye waweze kushika nafasi za wataalam kutoka nje ya nchi kwenye Ofisi za Tume ya Madini mapema kama Sheria ya Madini inavyowataka.

Aliendelea kufafanua kuwa, Serikali inapenda kuona wawekezaji katika sekta ya madini wanafanya kazi katika mazingira mazuri ili waweze kulipa kodi mbalimbali Serikalini.

“Ndio maana tozo nyingi zilizokuwepo kwenye madini ya chumvi zimeondolewa, tunataka mzalishe kwa faida, lakini wito wangu kwenu ni kuhakikisha mnafuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, Tume ya Madini ipo tayari kuwasaidia muda wowote,” alisisitiza Dkt. Macheyeki.

Awali akizungumzia changamoto za kampuni hiyo, mmoja wa wataalam kutoka kampuni hiyo, Tanmay Purohit alisema kuwa kumekuwepo na changamoto ya kukatika kwa umeme na kuongeza kuwa wameshaiomba Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuwekewa umeme katika mashamba ya chumvi yaliyopo katika eneo la Shungubweni wilayani humo na kuwekewa gesi kwa ajili ya matumizi ya kiwandani hapo.

Alisema kuwa wamekuwa wakitumia gharama kubwa ya kuendesha mitambo kwa kutumia dizeli pindi umeme unapokatika kiwandani hapo na katika mashamba ya chumvi.

No comments:

Powered by Blogger.