LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yasaidia mazishi ya watu 19 waliofariki kwa ajali ya gari mkoani Songwe

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Sehemu ya majeneza ya miili ya watu 19 yaliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe kufuatia ajali iliyohusisha magari matatu, mkoa pia umewezesha usafiri wa miili ya marehemu hao.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19.
Ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19 wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela akitoa salamu za pole.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela akikagua majeneza kabla hayajakabidhiwa kwa wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19.

RS Songwe
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela anatoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19 ikiwa wanaume ni 15 na wanawake wanne. 

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema kutokana na ajali hiyo iliyotokea jana usiku eneo la Senjele Wilayani Mbozi ikihusisha magari matatu yaliyokuwa yakielekea Mbeya kugongana, serikali mkoani Songwe imetoa majeneza 19 pamoja na usafiri kwa ajili ya kuhifadhi miili ya marehemu. 

“Rais Magufuli amenituma niwape pole na ametuelekeza kama Mkoa kusimamia Mamlaka za Usalama barabarani kufanya uchunguzi na hatua zinazo stahili kuchukuliwa, pia ameelekeza tujipange vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani”, amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela. 

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema chanzo cha ajali hiyo kimetokana na gari la abiria aina ya Coaster kugongwa na gari la mizigo lililokuwa nyuma yake kisha coaster kugonga gari la mizigo lililo kuwa mbele yake na kupelekea gari la abiria kubanwa katikati ya magari mawili ya mizigo. 

Aidha ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, kuweka utaratibu maalumu wa magari kupita kwa kupokezana katika maeneo yote yenye miteremko mikali, kuwepo ukaguzi wa magari kabla hayajaanza kushuka au kupanda mlima pamoja na kuweka ulinzi wa maeneo hayo. 

“Mungu ametupa akili za kufanya kazi na akili hizi tuzitumie kuzuia ajali ndani ya Mkoa wa Songwe, hivyo nawasihi watumiaji wote wa vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuweza kuepuka ajali kama hizi”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela. 

Mapema jana Brig. Jen. (Mst) Mwangela amefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songwe ambapo miili ya marehemu ilikuwa imehifadhiwa ili kuwafariji wafiwa waliofika kutambua miili ya ndugu zao.

No comments:

Powered by Blogger.