LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanahabari mkoani Tabora wapigwa msasa kuhusu afya uzazi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Mradi wa USAID Tulonge Afya fhi 360 imetoa mafunzo kwa wanahabari mkoani Tabora juu ya utoaji habari baada ya uzinduzi wa majukwaa mawili ya mawasiliano ya afya kwa watu wazima "NAWEZA" na vijana "SITETELEKI".

Majukwaa hayo yanalenga kufikisha elimu sahihi itakayoijengea jamii ya watanzania uwezo ili kubadilisha mitizamo na tabia zao za kiafya na kuleta matokeo chanya.

Mafunzo hayo yaliendeshwa jana na wataalamu wa masuala ya afya kutoka Wizara ya Afya na USAID Tulonge Afya fhi 360 katika Hotel ya Rastalemi mjini Tabora na kupata mwitikio mkubwa na uelewa mzuri kwa wanahabari wa mkoani humu yakiwa ni maandalizi ya uzinduzi wa majukwaa hayo ya NAWEZA na SITETEREKI mkoani humo.

Mtaalamu wa mambo ya Afya kutoka Wizara ya Afya, Oscar Kapera alisema NAWEZA ni jukwaa linalolenga kuwafikia wananchi tofauti tofauti na itachangia kuboresha afya na ustawi wa Watanzania wengi, itakuwa ikibadilika badilika ili kukidhi mahitaji ya maeneo mengine ya kiafya muhimu kwa walengwa hao ama makundi mengine hususani watu wazima.

Alisema kuwa vyombo vya habari vina ushawishi mkubwa kwenye jamii hivyo kupitia kwao elimu itawafikia walengwa na mipango ya serikali itatekelezwa kwa ufanisi na kufanikiwa.

Oscar alisema wanawake milioni 2 hujifungua kwa mwaka lakini ni asilimia 34 hufika vituo vya afya kupata huduma baada ya kujifungua hivyo jamii inatakiwa kupata elimu zaidi ili wahamasishe akina mama kujifungulia vituo na kupata huduma kwa wakati.

“NAWEZA inataka kujenga uwezo wa jamii kwa kuwapa elimu na taarifa sahihi za masuala ya afya ya uzazi na afya ya mama na mtoto na kubadilisha mitizamo na tabia na kuchochea kuleta matokeo chanya ya afya katika jamii, wajue jinsi ya kujikinga na maambukizi ya VVU na malaria,”alisema Oscar.

Aidha Oscar alisema jukwaa la SITETELEKI litawafikia vijana wenye umri kati ya 15 – 24, kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi zinazowakwamisha na kuwafanya washindwe kufikia malengo yao ya maisha.

Alisema vijana wanayo mitizamo tofauti hivyo jukwaa hilo litatumika kuwapa taarifa sahihi, wataungwa mkono na wazazi ili hatimaye wafanye uamuzi sahihi ili kufikia ndoto zao.

"Vijana wana changamoto nyingi za kiafya (mimba za utotoni na mamabukizi ya virusi vya Ukimwi) ndiyo maana serikali inataka kuona nguvu kazi hiyo inaokolewa na kufika inakotaka, wasichanganywe na mambo hasi ili waishi katika malengo na mtizamo huo watimize ndoto zao". Alisema Oscar.

Alieleza kuwa SITETEREKI itawafanya vijana wasitetereke bali wajitambue na kuzikabili changamoto zao kwa kupaza sauti, watumie huduma za uzazi kwa usahihi, wapime afya zao na kutambua kama wameambukizwa lakini pia wa kiume wafanyiwe tohara ya hiari kuepuka kuambukizwa VVU na wazazi wawaeleze ukweli vijana. 
Uwasilishaji mada ukiendelea kwenye mafunzo hayo.
BMG Habari

No comments:

Powered by Blogger.